Zaburi 12
Kuomba msaada 
 Kwa mwimbishaji. Mtindo wa sheminithi. Zaburi ya Daudi. 
  1 Mwenyezi Mungu tusaidie, kwa kuwa wacha Mungu wametoweka;  
waaminifu wametoweka miongoni mwa wanadamu.   
 2 Kila mmoja humwambia jirani yake uongo;  
midomo yao ya hila huzungumza kwa udanganyifu.   
 3 Mwenyezi Mungu na akatilie mbali midomo yote ya hila  
na kila ulimi uliojaa majivuno,   
 4 ule unaosema, “Kwa ndimi zetu tutashinda;  
midomo ni mali yetu, bwana wetu ni nani?”   
 5 “Kwa sababu wanyonge wanaonewa,  
na wahitaji wanalia kwa uchungu,  
nitainuka sasa,” asema Mwenyezi Mungu.  
“Nitawalinda kutokana na wale  
wenye nia mbaya juu yao.”   
 6 Maneno ya Mwenyezi Mungu ni safi,  
kama fedha iliyosafishwa katika tanuru,  
iliyosafishwa mara saba.   
 7 Ee Mwenyezi Mungu, utatuweka salama  
na kutulinda na kizazi hiki milele.   
 8 Watu waovu huenda wakiringa kila mahali  
wakati yule aliye mbaya sana  
ndiye anayeheshimiwa miongoni mwa watu.