Zaburi 13
Sala ya kuomba msaada
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi.
Hadi lini, Ee Mwenyezi Mungu? Je, utanisahau milele?
Utanificha uso wako hadi lini?
Nitapambana na mawazo yangu hadi lini,
na kila siku kuwa na majonzi moyoni mwangu?
Adui zangu watanishinda hadi lini?
 
Nitazame, unijibu, Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wangu.
Yatie nuru macho yangu,
ama sivyo nitalala usingizi wa mauti.
Adui yangu atasema, “Nimemshinda,”
nao adui zangu watashangilia nitakapoanguka.
 
Lakini ninategemea upendo wako usiokoma;
moyo wangu unashangilia katika wokovu wako.
Nitamwimbia Mwenyezi Mungu,
kwa kuwa amekuwa mwema kwangu.