Zaburi 14
Uovu wa wanadamu
(Zaburi 53)
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi.
Mpumbavu anasema moyoni mwake,
“Hakuna Mungu.”
Wamepotoka, matendo yao ni maovu kabisa;
hakuna hata mmoja atendaye mema.
 
Mwenyezi Mungu anawachungulia wanadamu
kutoka mbinguni
aone kama kuna mwenye hekima,
yeyote anayemtafuta Mungu.
Wote wamepotoka,
wote wameoza pamoja;
hakuna atendaye mema,
naam, hakuna hata mmoja!
 
Je, watendao maovu kamwe hawatajifunza:
wale ambao huwala watu wangu
kama watu walavyo mkate,
hao ambao hawamwiti Mwenyezi Mungu?
Wako hapo, wameingiwa na hofu kuu,
maana Mungu yupo pamoja na wenye haki.
Ninyi watenda maovu mnakwamisha mipango ya maskini,
bali Mwenyezi Mungu ndiye kimbilio lao.
 
Laiti wokovu wa Israeli
ungekuja kutoka Sayuni!
Mwenyezi Mungu anaporejesha
wafungwa wa watu wake,
Yakobo na ashangilie,
Israeli na afurahi!