Zaburi 15
Kitu Mwenyezi Mungu anachotaka
Zaburi ya Daudi.
1 Mwenyezi Mungu, ni nani awezaye kukaa
katika Hekalu lako?
Nani awezaye kuishi
katika mlima wako mtakatifu?
2 Ni yule aendaye pasipo mawaa,
atendaye yaliyo haki,
asemaye kweli toka moyoni mwake,
3 na hana masingizio ulimini mwake,
asiyemtenda jirani yake vibaya,
na asiyemsingizia mwenzake,
4 ambaye humdharau mtu mbaya,
lakini huwaheshimu wale wamwogopao Mwenyezi Mungu,
yule atunzaye kiapo chake
hata kama anaumia.
5 Yeye akopeshaye fedha yake bila riba,
na hapokei rushwa dhidi ya mtu asiye na hatia.
Mtu afanyaye haya
kamwe hatatikisika.