Zaburi 16
Sala ya matumaini
Utenzi wa Daudi.
1 Ee Mungu, uniweke salama,
kwa maana kwako nimekimbilia.
2 Nilimwambia Mwenyezi Mungu, “Wewe ndiwe Bwana wangu;
pasipo wewe sina jambo jema.”
3 Kuhusu watakatifu walio duniani,
hao ndio wenye fahari,
na ninapendezwa nao.
4 Huzuni itaongezeka kwa wale
wanaokimbilia miungu mingine.
Sitazimimina sadaka za damu kwa miungu kama hiyo,
au kutaja majina yao mdomoni mwangu.
5 Mwenyezi Mungu umeniwekea fungu langu na kikombe changu;
umeyafanya mambo yangu yote yawe salama.
6 Alama za mipaka zimeniangukia mahali pazuri,
hakika nimepata urithi mzuri.
7 Nitamsifu Mwenyezi Mungu ambaye hunishauri,
hata wakati wa usiku moyo wangu hunifundisha.
8 Nimemweka Mwenyezi Mungu mbele yangu daima.
Kwa sababu yuko mkono wangu wa kuume,
sitatikisika.
9 Kwa hiyo moyo wangu unafurahia,
na ulimi wangu unashangilia;
mwili wangu nao
utapumzika salama,
10 kwa maana hutaniacha Kuzimu*Kuzimu kwa Kiebrania ni Sheol, yaani Shimo lisilo na mwisho.,
wala hutamwacha Mtakatifu Wako
kuona uharibifu.
11 Umenijulisha njia ya uzima;
utanijaza na furaha mbele zako,
pamoja na furaha ya milele
katika mkono wako wa kuume.