Zaburi 18
Wimbo wa Daudi wa ushindi
(2 Samweli 22:1-51)
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi mtumishi wa Mwenyezi Mungu aliyomwimbia Mwenyezi Mungu alipomwokoa mikononi mwa adui zake wote, na pia mkononi mwa Sauli. Alisema hivi:
1 Nakupenda wewe, Ee Mwenyezi Mungu,
nguvu yangu.
2 Mwenyezi Mungu ni mwamba wangu,
ngome yangu na mwokozi wangu;
Mungu wangu ni mwamba wangu,
ninayemkimbilia.
Yeye ni ngao yangu na pembe*pembe inamaanisha nguvu ya wokovu wangu,
ngome yangu.
3 Ninamwita Mwenyezi Mungu anayestahili kusifiwa,
nami ninaokolewa kutoka kwa adui zangu.
4 Kamba za mauti zilinizunguka,
mafuriko ya maangamizi yalinilemea.
5 Kamba za Kuzimu zilinizunguka,
mitego ya mauti ilinikabili.
6 Katika shida yangu nalimwita Mwenyezi Mungu,
nilimlilia Mungu wangu anisaidie.
Kutoka hekaluni mwake alisikia sauti yangu,
kilio changu kikafika mbele zake,
masikioni mwake.
7 Dunia ilitetemeka na kutikisika,
misingi ya milima ikatikisika;
vilitetemeka kwa sababu alikuwa amekasirika.
8 Moshi ukapanda kutoka puani mwake,
moto uteketezao ukatoka kinywani mwake,
makaa ya moto yanayowaka
yakatoka ndani yake.
9 Akazipasua mbingu akashuka chini,
mawingu meusi yalikuwa chini ya miguu yake.
10 Alipanda juu ya kerubi akaruka,
akapaa juu kwa mabawa ya upepo.
11 Alifanya giza kuwa kitu chake cha kujifunika,
hema lake kumzunguka:
mawingu meusi ya mvua ya angani.
12 Kutokana na mwanga wa uwepo wake
mawingu yalisogea,
ikashuka mvua ya mawe
na miali ya radi.
13 Mwenyezi Mungu alinguruma kutoka mbinguni,
sauti ya Aliye Juu Sana ilisikika.
14 Aliipiga mishale yake na kutawanya adui,
naam, umeme mwingi wa radi na kuwafukuza.
15 Mabonde ya bahari yalifunuliwa,
na misingi ya dunia ikawa wazi
kwa kukaripia kwako, Ee Mwenyezi Mungu,
kwa uvumi wa pumzi kutoka puani mwako.
16 Alinyoosha mkono kutoka juu na kunishika;
alinitoa kilindini cha maji makuu.
17 Aliniokoa kutoka adui yangu mwenye nguvu nyingi,
kutoka adui zangu waliokuwa na nguvu nyingi kuliko mimi.
18 Walinikabili siku ya msiba wangu,
lakini Mwenyezi Mungu alikuwa msaada wangu.
19 Alinileta nje mahali penye nafasi tele,
akaniokoa kwa kuwa alipendezwa nami.
20 Mwenyezi Mungu alinitendea sawasawa na uadilifu wangu;
amenilipa sawasawa na usafi wa mikono yangu.
21 Kwa maana nimezishika njia za Mwenyezi Mungu;
sijatenda ubaya nikamwacha Mungu wangu.
22 Sheria zake zote zi mbele yangu,
wala sijayaacha maagizo yake.
23 Nimekuwa sina hatia mbele zake,
nami nimejilinda nisitende dhambi.
24 Mwenyezi Mungu amenilipa sawasawa na uadilifu wangu;
sawasawa na usafi wa mikono yangu machoni pake.
25 Kwa yeye aliye mwaminifu, unajionesha kuwa mwaminifu,
kwa asiye na hatia, unajionesha kutokuwa na hatia.
26 Kwa aliye mtakatifu, unajionesha kuwa mtakatifu,
lakini kwa aliyepotoka, unajionesha kuwa mkaidi.
27 Wewe huwaokoa wanyenyekevu,
lakini huwashusha wenye kiburi.
28 Wewe, Ee Mwenyezi Mungu, unaifanya taa yangu iendelee kuwaka;
Mungu wangu hulifanya giza langu kuwa mwanga.
29 Kwa msaada wako naweza kushinda jeshi,
nikiwa pamoja na Mungu wangu
nitaweza kuruka ukuta.
30 Kuhusu Mungu, njia yake ni kamilifu,
neno la Mwenyezi Mungu halina dosari.
Yeye ni ngao kwa wote
wanaokimbilia kwake.
31 Kwa maana ni nani aliye Mungu
zaidi ya Mwenyezi Mungu?
Ni nani aliye Mwamba
isipokuwa Mungu wetu?
32 Mungu ndiye anivikaye nguvu
na kufanya njia yangu kuwa kamilifu.
33 Huifanya miguu yangu kama miguu ya kulungu,
huniwezesha kusimama mahali palipo juu.
34 Huifundisha mikono yangu kupigana vita;
mikono yangu inaweza kupinda upinde wa shaba.
35 Hufanya msaada wa wokovu wako kuwa ngao yangu,
nao mkono wako wa kuume hunitegemeza;
msaada wako umeniinua niwe mkuu.
36 Huyapanua mapito yangu,
ili miguu yangu isiteleze.
37 Niliwafuatia adui zangu na nikawapata,
sikurudi nyuma hadi walipoangamizwa.
38 Niliwaseta hata hawakuweza kuinuka tena;
walianguka chini ya miguu yangu.
39 Ulinivika nguvu kwa ajili ya kupigana vita;
uliwafanya adui zangu wasujudu miguuni pangu.
40 Uliwafanya adui zangu wageuke na kukimbia,
nami nikawaangamiza adui zangu.
41 Walipiga yowe, lakini hapakuwa na mtu wa kuwaokoa;
walimlilia Mwenyezi Mungu, lakini hakuwajibu.
42 Niliwaponda kama mavumbi yanayopeperushwa na upepo;
niliwamwaga nje kama tope barabarani.
43 Umeniokoa kutokana na mashambulizi ya watu;
umenifanya kiongozi wa mataifa;
watu ambao sikuwajua wananitumikia.
44 Mara wanisikiapo hunitii,
wageni hunyenyekea mbele yangu.
45 Wote wanalegea,
wanatoka katika ngome zao wakitetemeka.
46 Mwenyezi Mungu yu hai! Sifa ni kwa Mwamba wangu!
Atukuzwe Mungu Mwokozi wangu!
47 Yeye ndiye Mungu anilipiziaye kisasi,
awatiishaye mataifa chini yangu,
48 aniokoaye na adui zangu.
Uliniinua juu ya adui zangu;
uliniokoa toka kwa watu wajeuri.
49 Kwa hiyo nitakusifu katika mataifa, Ee Mwenyezi Mungu;
nitaliimbia sifa jina lako.
50 Humpa mfalme wake ushindi mkuu,
huonesha fadhili zake kwa mpakwa mafuta wake,
kwa Daudi na wazao wake milele.