Zaburi 19
Utukufu wa Mwenyezi Mungu katika uumbaji
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi.
Mbingu zinatangaza utukufu wa Mungu,
anga zahubiri kazi ya mikono yake.
Siku baada ya siku zinatoa habari,
usiku baada ya usiku zinatangaza maarifa.
Hakuna msemo wala lugha,
ambapo sauti zao hazisikiki.
Sauti yao imeenea duniani pote,
nayo maneno yao yameenea
hadi miisho ya ulimwengu.
 
Katika mbingu amepiga hema kwa ajili ya jua,
linafanana na bwana arusi
akitoka chumbani mwake,
kama shujaa anavyofurahia
kukamilisha kushindana kwake.
Huchomoza upande mmoja wa mbingu,
na kufanya mzunguko wake
hadi upande mwingine.
Hakuna kilichojificha joto lake.
 
Torati ya Mwenyezi Mungu ni kamilifu,
ikihuisha nafsi.
Shuhuda za Mwenyezi Mungu ni za kuaminika,
zikimpa mjinga hekima.
Maagizo ya Mwenyezi Mungu ni kamili,
nayo hufurahisha moyo.
Amri za Mwenyezi Mungu huangaza,
zatia nuru machoni.
Kumcha Mwenyezi Mungu ni utakatifu,
nako kwadumu milele.
Amri za Mwenyezi Mungu ni za hakika,
nazo zina haki.
10 Ni za thamani kuliko dhahabu,
kuliko dhahabu iliyo safi sana,
ni tamu kuliko asali,
kuliko asali kutoka sega.
11 Kwa hizo mtumishi wako anaonywa,
katika kuzishika kuna thawabu kubwa.
 
12 Ni nani awezaye kutambua makosa yake?
Nisamehe makosa yangu nisiyoyajua.
13 Mlinde mtumishi wako na dhambi za makusudi,
nazo zisinitawale.
Ndipo nitakapokuwa sina lawama,
niwe huru na hatia kubwa.
 
14 Maneno ya kinywa changu
na mawazo ya moyo wangu,
yapate kibali mbele zako, Ee Mwenyezi Mungu,
Mwamba wangu na Mkombozi wangu.