Zaburi 20
Maombi kwa ajili ya ushindi
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi.
Mwenyezi Mungu na akujibu unapokuwa katika dhiki,
jina la Mungu wa Yakobo na liwe kinga yako.
Na akutumie msaada kutoka patakatifu
na akupatie msaada kutoka Sayuni.
Na azikumbuke dhabihu zako zote,
na azikubali sadaka zako za kuteketezwa.
Na akujalie haja ya moyo wako,
na aifanikishe mipango yako yote.
Tutashangilia kwa furaha utakaposhinda,
tutainua bendera zetu kwa jina la Mungu wetu.
Mwenyezi Mungu na akupe haja zako zote.
 
Sasa nafahamu kuwa Mwenyezi Mungu
humwokoa mpakwa mafuta wake,
humjibu kutoka mbingu yake takatifu
kwa nguvu za wokovu wa mkono wake wa kuume.
Wengine wanatumaini magari ya vita, na wengine farasi,
bali sisi tutalitumainia jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wetu.
Wao wameshushwa chini na kuanguka,
bali sisi tunainuka na kusimama imara.
 
Ee Mwenyezi Mungu, mwokoe mfalme!
Tujibu tunapokuita!