Zaburi 22
Kilio cha uchungu na wimbo wa sifa 
 Kwa mwimbishaji. Mtindo wa utenzi wa “Kulungu wa Alfajiri”. Zaburi ya Daudi. 
  1 Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?  
Kwa nini uko mbali hivyo kuniokoa?  
Mbali hivyo na maneno ya kuugua kwangu?   
 2 Ee Mungu wangu, ninalia mchana, lakini hunijibu,  
hata usiku, sinyamazi.   
 3 Hata hivyo umesimikwa kwenye kiti cha enzi,  
Wewe Uliye Mtakatifu;  
wewe ni sifa ya Israeli.*Tafsiri zingine zinasema uketiye juu ya sifa za Israeli.   
 4 Kwako wewe baba zetu waliweka tumaini lao,  
walikutumaini nawe ukawaokoa.   
 5 Walikulilia wewe na ukawaokoa,  
walikutegemea wewe nao hawakuaibika.   
 6 Mimi ni mnyoo wala si mwanadamu,  
wanaume wamenibeza, na watu wamenidharau.   
 7 Wote wanaoniona wananidhihaki;  
wananivurumishia matusi, wakitikisa vichwa vyao:   
 8 Wanasema, “Amtegemea Mwenyezi Mungu,  
basi Mwenyezi Mungu na amwokoe.  
Amkomboe basi, kwa maana  
anapendezwa naye.”   
 9 Hata hivyo ulinitoa tumboni,  
ukanifanya nikutegemee,  
hata nilipokuwa ninanyonya  
matiti ya mama yangu.   
 10 Nimekabidhiwa kwako tangu kuzaliwa,  
toka tumboni mwa mama yangu  
umekuwa Mungu wangu.   
 11 Usiwe mbali nami,  
kwa maana shida iko karibu  
na hakuna wa kunisaidia.   
 12 Mafahali wengi wamenizunguka,  
mafahali wa Bashani wenye nguvu  
wamenizingira.   
 13 Simba wanaonguruma na kurarua mawindo  
wanapanua vinywa vyao dhidi yangu.   
 14 Nimemiminwa kama maji,  
mifupa yangu yote imeteguka viungoni.  
Moyo wangu umegeuka kuwa nta,  
umeyeyuka ndani yangu.   
 15 Nguvu zangu zimekauka kama kigae,  
ulimi wangu umegandamana  
na kaakaa la kinywa changu,  
kwa sababu umenilaza  
katika mavumbi ya kifo.   
 16 Mbwa wamenizunguka,  
kundi la watu waovu limenizingira;  
wamenidunga mikono na miguu.   
 17 Naweza kuhesabu mifupa yangu yote,  
watu wananikodolea macho na kunisimanga.   
 18 Wanagawana nguo zangu,  
na vazi langu wanalipigia kura.   
 19 Lakini wewe, Ee Mwenyezi Mungu,  
usiwe mbali.  
Ee Nguvu yangu,  
uje haraka unisaidie.   
 20 Okoa maisha yangu na upanga,  
uhai wangu wa thamani kutoka nguvu za mbwa.   
 21 Niokoe kutoka kinywani mwa simba,  
niokoe kutoka pembe za nyati.   
 22 Nitalitangaza jina lako kwa ndugu zangu,  
katika kusanyiko nitakusifu wewe.   
 23 Ninyi ambao mnamcha Mwenyezi Mungu, msifuni!  
Ninyi nyote wazao wa Yakobo, mheshimuni yeye!  
Mcheni yeye, ninyi wazao wa Israeli!   
 24 Kwa maana hakupuuza wala kudharau  
mateso ya aliyeteswa;  
hakumficha uso wake  
bali alisikiliza kilio chake.   
 25 Kwako wewe hutoka kiini cha sifa zangu katika kusanyiko kubwa,  
nitatimiza nadhiri zangu mbele ya wale wanaokucha wewe.   
 26 Maskini watakula na kushiba,  
wale wanaomtafuta Mwenyezi Mungu watamsifu:  
mioyo yenu na iishi milele!   
 27 Miisho yote ya dunia itakumbuka  
na kumgeukia Mwenyezi Mungu,  
nazo jamaa zote za mataifa  
zitasujudu mbele zake,   
 28 kwa maana ufalme ni wa Mwenyezi Mungu  
naye huyatawala mataifa.   
 29 Matajiri wote wa dunia watasherehekea na kuabudu.  
Wote wanaoshuka mavumbini  
watapiga magoti mbele yake,  
wote ambao hawawezi  
kudumisha uhai wao.   
 30 Wazao wa baadaye watamtumikia yeye;  
vizazi vijavyo vitajulishwa habari za Bwana.   
 31 Watatangaza haki yake kwa watu  
ambao hawajazaliwa bado,  
kwa maana yeye ametenda hili.