Zaburi 24
Mfalme mkuu
Zaburi ya Daudi.
1 Dunia ni mali ya Mwenyezi Mungu, na vyote vilivyomo,
ulimwengu, na wote wanaoishi ndani yake,
2 maana aliiwekea misingi yake baharini,
na kuifanya imara juu ya maji.
3 Nani awezaye kuupanda mlima wa Mwenyezi Mungu?
Ni nani awezaye kusimama patakatifu pake?
4 Ni yule mwenye mikono safi na moyo mweupe,
yule ambaye hakuinulia sanamu nafsi yake
au kuapa kwa kitu cha uongo.
5 Huyo atapokea baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu,
na hukumu ya haki kutoka kwa Mungu Mwokozi wake.
6 Hiki ndicho kizazi cha wale wanaomtafuta,
wale wanaoutafuta uso wako, Ee Mungu wa Yakobo.
7 Inueni vichwa vyenu, enyi malango,
inukeni enyi milango ya kale,
ili mfalme wa utukufu apate kuingia.
8 Ni nani huyu Mfalme wa utukufu?
Ni Mwenyezi Mungu aliye na nguvu na uweza,
ni Mwenyezi Mungu aliye hodari katika vita.
9 Inueni vichwa vyenu, enyi malango,
viinueni juu enyi milango ya kale,
ili Mfalme wa utukufu apate kuingia.
10 Ni nani yeye, huyu Mfalme wa utukufu?
Ni Mwenyezi Mungu,
Mungu wa majeshi ya mbinguni;
yeye ndiye Mfalme wa utukufu.