Zaburi 28
Kuomba msaada
Zaburi ya Daudi.
Ninakuita wewe, Ee Mwenyezi Mungu, Mwamba wangu;
usikatae kunisikiliza.
Kwa sababu ukinyamaza
nitafanana na walioshuka shimoni.
Sikia kilio changu nikikuomba unihurumie,
ninapokuita ili unisaidie,
ninapoinua mikono yangu kuelekea
Patakatifu pa Patakatifu pako.
 
Usiniburute pamoja na waovu,
pamoja na hao watendao mabaya,
ambao huzungumza na majirani zao maneno mazuri,
lakini mioyoni mwao wameficha chuki.
Walipe sawasawa na matendo yao,
sawasawa na matendo yao maovu;
walipe sawasawa na kazi za mikono yao,
uwalipe wanavyostahili.
Kwa kuwa hawaheshimu kazi za Mwenyezi Mungu,
na yale ambayo mikono yake imetenda,
atawabomoa na kamwe
hatawajenga tena.
 
Ahimidiwe Mwenyezi Mungu,
kwa maana amesikia kilio changu
nikimwomba anihurumie.
Mwenyezi Mungu ni nguvu zangu na ngao yangu,
moyo wangu umemtumaini yeye,
nami nimesaidiwa.
Moyo wangu unarukaruka kwa furaha
nami nitamshukuru kwa wimbo.
 
Mwenyezi Mungu ni nguvu ya watu wake,
ngome ya wokovu kwa mpakwa mafuta wake.
Waokoe watu wako na uubariki urithi wako;
uwe mchungaji wao na uwabebe milele.