Zaburi 29
Sauti ya Mwenyezi Mungu wakati wa dhoruba
Zaburi ya Daudi.
1 Mpeni Mwenyezi Mungu, enyi mashujaa,
mpeni Mwenyezi Mungu utukufu na nguvu.
2 Mpeni Mwenyezi Mungu utukufu unaostahili jina lake;
mwabuduni Mwenyezi Mungu katika uzuri wa utakatifu wake.
3 Sauti ya Mwenyezi Mungu iko juu ya maji;
Mungu wa utukufu hupiga radi,
Mwenyezi Mungu hupiga radi juu ya maji makuu.
4 Sauti ya Mwenyezi Mungu ina nguvu;
sauti ya Mwenyezi Mungu ni tukufu.
5 Sauti ya Mwenyezi Mungu huvunja mierezi;
Mwenyezi Mungu huvunja vipande vipande
mierezi ya Lebanoni.
6 Hufanya Lebanoni irukaruke kama ndama,
Sirioni*yaani Mlima Hermoni urukaruke kama mwana nyati.
7 Sauti ya Mwenyezi Mungu hupiga
kwa miali ya radi.
8 Sauti ya Mwenyezi Mungu hutikisa jangwa;
Mwenyezi Mungu hutikisa Jangwa la Kadeshi.
9 Sauti ya Mwenyezi Mungu huzalisha ayala,
na huuacha msitu wazi.
Hekaluni mwake wote wasema,
“Utukufu!”
10 Mwenyezi Mungu huketi akiwa ametawazwa juu ya gharika;
Mwenyezi Mungu ametawazwa kuwa Mfalme milele.
11 Mwenyezi Mungu huwapa watu wake nguvu;
Mwenyezi Mungu huwabariki watu wake kwa kuwapa amani.