Zaburi 30
Maombi ya shukrani
Utenzi wa kuweka wakfu hekalu. Zaburi ya Daudi.
1 Nitakutukuza wewe, Ee Mwenyezi Mungu,
kwa kuwa umeniinua kutoka vilindi,
na hukuacha adui zangu
washangilie juu yangu.
2 Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, nilikuita unisaidie
na wewe umeniponya.
3 Ee Mwenyezi Mungu, umenitoa Kuzimu*Kuzimu kwa Kiebrania ni Sheol, yaani Shimo lisilo na mwisho.,
umeniokoa nisishuke kwenye shimo la mauti.
4 Mwimbieni Mwenyezi Mungu, enyi watakatifu wake;
lisifuni jina lake takatifu.
5 Kwa maana hasira yake ni ya muda mfupi,
bali upendo wake hudumu siku zote.
Inawezekana kilio kiwepo usiku kucha,
lakini furaha huja asubuhi.
6 Nilipofanikiwa nilisema,
“Sitatikiswa kamwe.”
7 Ee Mwenyezi Mungu, uliponijalia,
uliuimarisha mlima wangu,
lakini ulipouficha uso wako
nilifadhaika.
8 Kwako wewe, Ee Mwenyezi Mungu, niliita,
niliomba rehema kwa Bwana:
9 “Kuna faida gani katika kuangamia kwangu,
katika kushuka kwangu shimoni?
Je, mavumbi yatakusifu?
Je, yatatangaza uaminifu wako?
10 Ee Mwenyezi Mungu, unisikie na kunihurumia;
Ee Mwenyezi Mungu, uwe msaada wangu.”
11 Uligeuza maombolezo yangu kuwa kucheza,
ulinivua gunia ukanivika shangwe,
12 ili moyo wangu uweze kukusifu na usikae kimya.
Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, nitakushukuru milele.