Zaburi 31
Maombi na sifa kwa kuokolewa kutoka kwa adui
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi.
1 Ee Mwenyezi Mungu, nimekukimbilia wewe,
usiache nikaaibika kamwe,
kwa haki yako uniokoe.
2 Nitegee sikio lako,
uje uniokoe haraka;
uwe kwangu mwamba wa kimbilio,
ngome imara ya kuniokoa.
3 Kwa kuwa wewe ni mwamba wangu na ngome yangu,
uniongoze na kunilinda kwa ajili ya jina lako.
4 Uniepushe na mtego niliotegewa,
maana wewe ndiwe kimbilio langu.
5 Ninaikabidhi roho yangu mikononi mwako,
unikomboe Ee Mwenyezi Mungu, uliye Mungu wa kweli.
6 Ninawachukia wale wanaoshikilia sanamu batili;
bali mimi ninamtumaini Mwenyezi Mungu.
7 Nitafurahia na kushangilia upendo wako,
kwa kuwa uliona mateso yangu
na ulijua maumivu ya nafsi yangu.
8 Hukunikabidhi kwa adui yangu
bali umeiweka miguu yangu mahali penye nafasi.
9 Ee Mwenyezi Mungu unihurumie, kwa kuwa niko kwenye shida;
macho yangu yanafifia kwa huzuni,
nafsi yangu na mwili wangu kwa sikitiko.
10 Maisha yangu yamedhoofika kwa majonzi,
naam, miaka yangu kwa kulia kwa maumivu makali;
nguvu zangu zinaisha kwa ajili ya mateso,
na mifupa yangu inachakaa.
11 Kwa sababu ya adui zangu wote,
nimedharauliwa kabisa na majirani zangu,
hata kwa rafiki zangu nimekuwa tisho,
wale wanaoniona barabarani wananikimbia.
12 Nimesahaulika miongoni mwao kama mtu aliyekufa,
nimekuwa kama chombo cha mfinyanzi kilichovunjika.
13 Kwa maana nimesikia maneno niliyosingiziwa na wengi;
vitisho viko pande zote;
kwa kuwa wamefanya mashauri dhidi yangu,
na kula njama kuniua.
14 Lakini mimi ninakutumaini wewe peke yako, Ee Mwenyezi Mungu;
nimesema, “Wewe ndiwe Mungu wangu.”
15 Siku za maisha yangu ziko mikononi mwako,
uniokoe mikononi mwa adui zangu
na wale wanifuatiao.
16 Mwangazie mtumishi wako uso wako,
uniokoe kwa ajili ya upendo wako usiokoma.
17 Usiniache niaibike, Ee Mwenyezi Mungu,
kwa maana nimekulilia wewe,
bali waovu waaibishwe
na kunyamazishwa Kuzimu.
18 Midomo yao isemayo uongo na inyamazishwe,
kwa maana kwa kiburi na dharau
wao husema kwa majivuno
dhidi ya wenye haki.
19 Tazama jinsi wema wako ulivyo mkuu,
uliowawekea akiba wanaokucha,
unaowapa wale wanaokukimbilia
machoni pa watu wote.
20 Unawahifadhi katika uvuli wa uwepo wako
kutokana na hila za wanadamu;
katika makao yako huwaweka salama
kutokana na ndimi za mashtaka.
21 Atukuzwe Mwenyezi Mungu,
kwa kuwa amenionesha upendo wake wa ajabu
nilipokuwa katika mji uliozingirwa.
22 Katika hofu yangu nilisema,
“Nimekatiliwa mbali na macho yako!”
Hata hivyo ulisikia kilio changu
ukanihurumia nilipokuita unisaidie.
23 Mpendeni Mwenyezi Mungu ninyi watakatifu wake wote!
Mwenyezi Mungu huwahifadhi waaminifu,
lakini wenye kiburi huwalipiza kikamilifu.
24 Kuweni hodari na mjipe moyo,
ninyi nyote mnaomtumaini Mwenyezi Mungu.