Zaburi 32
Furaha ya msamaha 
 Zaburi ya Daudi. Funzo. 
  1 Heri mtu aliyesamehewa makosa yake,  
ambaye dhambi zake zimefunikwa.   
 2 Heri mtu yule ambaye Mwenyezi Mungu  
hamhesabii dhambi,  
na ambaye rohoni mwake  
hamna udanganyifu.   
 3 Niliponyamaza, mifupa yangu ilichakaa  
kwa kulia kwa maumivu makali mchana kutwa.   
 4 Usiku na mchana  
mkono wako ulinilemea,  
nguvu zangu zilinyonywa  
kama vile katika joto la kiangazi.   
 5 Kisha nikakiri dhambi yangu kwako,  
wala sikuficha uovu wangu.  
Nilisema, “Nitaungama  
makosa yangu kwa Mwenyezi Mungu.”  
Ndipo uliponisamehe  
hatia ya dhambi yangu.   
 6 Kwa hiyo kila mtu mcha Mungu akuombe  
wakati unapopatikana,  
hakika maji makuu yatakapofurika  
hayatamfikia yeye.   
 7 Wewe ndiwe mahali pangu pa kujificha,  
utaniepusha na taabu  
na kunizunguka kwa nyimbo za wokovu.   
 8 Nitakufundisha na kukuonesha njia utakayoiendea;  
nitakushauri na kukuangalia.   
 9 Usiwe kama farasi au nyumbu  
wasio na akili,  
ambao ni lazima waongozwe kwa lijamu na hatamu  
la sivyo hawatakukaribia.   
 10 Mtu mwovu ana taabu nyingi,  
bali upendo usio na kikomo wa Mwenyezi Mungu  
unamzunguka mtu anayemtumaini.   
 11 Shangilieni katika Mwenyezi Mungu na mfurahi, enyi wenye haki!  
Imbeni, nyote mlio wanyofu wa moyo!