Zaburi 33
Ukuu na wema wa Mwenyezi Mungu
1 Mwimbieni Mwenyezi Mungu kwa furaha, enyi wenye haki;
wanyofu wa moyo wanapaswa kumsifu.
2 Msifuni Mwenyezi Mungu kwa kinubi,
mwimbieni sifa kwa zeze la nyuzi kumi.
3 Mwimbieni wimbo mpya;
pigeni kwa ustadi, na mpaze sauti za shangwe.
4 Maana neno la Mwenyezi Mungu ni haki na kweli,
ni mwaminifu kwa yote atendayo.
5 Mwenyezi Mungu hupenda uadilifu na haki;
dunia imejaa upendo wake usiokoma.
6 Kwa neno la Mwenyezi Mungu mbingu ziliumbwa,
jeshi lao la angani likaumbwa
kwa pumzi ya kinywa chake.
7 Anayakusanya maji ya bahari
kama kwenye chungu;
vilindi vya bahari
anaviweka katika ghala.
8 Dunia yote na imwogope Mwenyezi Mungu,
watu wote wa dunia wamche.
9 Kwa maana Mungu alisema, na ikawa,
aliamuru na ikasimama imara.
10 Mwenyezi Mungu huzuia mipango ya mataifa,
hupinga makusudi ya mataifa.
11 Lakini mipango ya Mwenyezi Mungu inasimama imara milele,
makusudi ya moyo wake kwa vizazi vyote.
12 Heri taifa ambalo Mwenyezi Mungu ni Mungu wao,
watu ambao aliwachagua kuwa urithi wake.
13 Mwenyezi Mungu hutazama chini kutoka mbinguni
na kuwaona wanadamu wote;
14 kutoka maskani mwake huwaangalia
wote wanaoishi duniani:
15 yeye ambaye huumba mioyo yao wote,
ambaye huangalia kila kitu wanachokitenda.
16 Hakuna mfalme anayeokoka kwa ukubwa wa jeshi lake;
hakuna shujaa anayeokoka kwa wingi wa nguvu zake.
17 Farasi ni tumaini la bure kwa wokovu,
licha ya nguvu zake nyingi, hawezi kuokoa.
18 Lakini macho ya Mwenyezi Mungu yako kwa wale wamchao,
kwa wale tumaini lao liko katika upendo wake usio na kikomo,
19 ili awaokoe na mauti,
na kuwahifadhi wakati wa njaa.
20 Sisi tunamngojea Mwenyezi Mungu kwa matumaini,
yeye ni msaada wetu na ngao yetu.
21 Mioyo yetu humshangilia,
kwa maana tunalitumainia jina lake takatifu.
22 Upendo wako usio na mwisho ukae juu yetu, Ee Mwenyezi Mungu,
tunapoliweka tumaini letu kwako.