Zaburi 34
Sifa na wema wa Mwenyezi Mungu
Zaburi ya Daudi, alipojifanya mwendawazimu mbele ya Abimeleki, ambaye alimfukuza, naye akaondoka.
1 Nitamtukuza Mwenyezi Mungu nyakati zote,
sifa zake zitakuwa mdomoni mwangu siku zote.
2 Nafsi yangu itajisifu katika Mwenyezi Mungu,
walioonewa watasikia na wafurahi.
3 Mtukuzeni Mwenyezi Mungu pamoja nami,
naam, na tulitukuze jina lake pamoja.
4 Nilimtafuta Mwenyezi Mungu naye akanijibu,
akaniokoa kwenye hofu zangu zote.
5 Wale wamtazamao hutiwa nuru,
nyuso zao hazifunikwi na aibu kamwe.
6 Maskini huyu alimwita Mwenyezi Mungu, naye akamsikia,
akamwokoa katika taabu zake zote.
7 Malaika wa Mwenyezi Mungu hufanya kituo
akiwazunguka wale wamchao,
naye huwaokoa.
8 Onjeni mwone kwamba Mwenyezi Mungu ni mwema;
heri mtu yule anayemkimbilia.
9 Mcheni Mwenyezi Mungu enyi watakatifu wake,
kwa maana wale wamchao
hawapungukiwi na chochote.
10 Wana simba wenye nguvu
hutindikiwa na kuona njaa,
bali wale wanaomtafuta Mwenyezi Mungu
hawatakosa kitu chochote kilicho chema.
11 Njooni, watoto wangu, mnisikilize,
nitawafundisha kumcha Mwenyezi Mungu.
12 Yeyote kati yenu anayependa uzima
na kutamani kuziona siku nyingi njema,
13 basi auzuie ulimi wake na mabaya,
na midomo yake kutokana na kusema uongo.
14 Aache uovu, atende mema,
aitafute amani na kuifuatilia.
15 Macho ya Mwenyezi Mungu huwaelekea wenye haki,
na masikio yake yako makini kusikiliza kilio chao.
16 Uso wa Mwenyezi Mungu uko kinyume na watendao maovu,
ili kufuta kumbukumbu lao duniani.
17 Wenye haki hulia, naye Mwenyezi Mungu huwasikia,
huwaokoa katika taabu zao zote.
18 Mwenyezi Mungu yu karibu na waliovunjika moyo,
na huwaokoa waliopondeka roho.
19 Mwenye haki ana mateso mengi,
lakini Mwenyezi Mungu humwokoa nayo yote,
20 huhifadhi mifupa yake yote,
hata mmoja hautavunjika.
21 Ubaya utamuua mtu mwovu,
nao adui za mwenye haki watahukumiwa.
22 Mwenyezi Mungu huwakomboa watumishi wake,
yeyote anayemkimbilia yeye
hatahukumiwa kamwe.
*^ Zaburi hii imetungwa kila mstari ukianzia na herufi ya alfabeti ya Kiebrania zikifuatana tangu Aleph (A) hadi Taw (T); zote ni 22.