Zaburi 35
Kuomba msaada: Kuokolewa kutokana na adui 
 Zaburi ya Daudi. 
  1 Ee Mwenyezi Mungu, pingana na wale wanaopingana nami,  
upigane na hao wanaopigana nami.   
 2 Chukua ngao na kigao.  
Inuka unisaidie.   
 3 Inua mkuki wako na fumo*Fumo ni sawa na sagai, yaani mkuki mfupi. lako  
dhidi ya hao wanaonifuatia.  
Iambie nafsi yangu,  
“Mimi ni wokovu wako.”   
 4 Wafedheheshwe na waaibishwe  
wale wanaotafuta uhai wangu.  
Wanaofanya shauri kuniangamiza  
wafukuzwe mbali kwa bumbuazi.   
 5 Wawe kama makapi yapeperushwayo na upepo,  
malaika wa Mwenyezi Mungu akiwafukuza.   
 6 Njia yao na iwe giza na ya utelezi,  
malaika wa Mwenyezi Mungu akiwafuatilia.   
 7 Kwa vile walinifichia wavu wao bila sababu,  
na bila sababu wamenichimbia shimo,   
 8 maafa na yawapate ghafula:  
wavu walionifichia na uwatege wenyewe,  
na waanguke katika shimo hilo,  
kwa maangamizi yao.   
 9 Ndipo nafsi yangu itashangilia katika Mwenyezi Mungu  
na kuufurahia wokovu wake.   
 10 Nitapaza sauti yangu nikisema,  
“Ni nani aliye kama wewe, Ee Mwenyezi Mungu?  
Wewe huwaokoa maskini kutokana na wale waliowazidi nguvu,  
unawaokoa maskini na wahitaji kutokana na wanaowanyang’anya!”   
 11 Mashahidi wakatili wanainuka,  
wananiuliza mambo nisiyoyajua.   
 12 Wananilipa baya kwa jema  
na kuiacha nafsi yangu ukiwa.   
 13 Lakini walipokuwa wagonjwa, nilivaa gunia  
na nikajinyenyekeza kwa kufunga.  
Maombi yangu yaliponirudia bila kujibiwa,   
 14 niliendelea kuomboleza  
kama vile wao ni rafiki au ndugu.  
Niliinamisha kichwa chini kwa huzuni  
kama ninayemwombolezea mama yangu.   
 15 Lakini nilipojikwaa,  
walikusanyika kwa shangwe;  
washambuliaji walijikusanya dhidi yangu  
bila mimi kujua.  
Walinisingizia pasipo kukoma.   
 16 Kama watu wasiomcha Mungu, wamenidhihaki,  
wamenisagia meno.   
 17 Ee Bwana, utatazama hadi lini?  
Niokoe maisha yangu na maangamizi yao,  
okoa uhai wangu wa thamani  
kutokana na simba hawa.   
 18 Nami nitakushukuru mbele ya kusanyiko kubwa,  
nitakusifu katikati ya watu wengi.   
 19 Usiwaache wale wanaonisimanga,  
wale ambao ni adui zangu bila sababu;  
usiwaache wale ambao ni adui zangu bila sababu  
wakonyeze jicho kwa hila.   
 20 Hawazungumzi kwa amani,  
bali wanatunga mashtaka ya uongo  
dhidi ya wale wanaoishi  
kwa utulivu katika nchi.   
 21 Hunifumbulia vinywa vyao wakisema, “Aha! Aha!  
Kwa macho yetu wenyewe tumeliona.”   
 22 Ee Mwenyezi Mungu, umeona hili, usiwe kimya.  
Usiwe mbali nami, Ee Bwana.   
 23 Amka, inuka unitetee!  
Unipiganie Mungu wangu na Bwana wangu.   
 24 Nihukumu kwa haki yako, Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wangu,  
sawasawa na haki yako;  
usiwaache wakusimange.   
 25 Usiwaache wafikiri, “Aha, hili ndilo tulilotaka!”  
Au waseme, “Tumemmeza.”   
 26 Wote wanaofurahia dhiki yangu  
waaibishwe na wachanganyikiwe;  
hao wanaojiinua dhidi yangu  
wavikwe aibu na dharau.   
 27 Wale wanaofurahia hukumu yangu ya haki  
wapige kelele za shangwe na furaha;  
hebu waseme siku zote, “Mwenyezi Mungu atukuzwe,  
ambaye amefurahia mafanikio ya mtumishi wake.”   
 28 Ulimi wangu utanena haki yako  
na sifa zako mchana kutwa.