Zaburi 36
Uovu wa mwanadamu 
 Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi mtumishi wa Mwenyezi Mungu. 
  1 Kuna neno moyoni mwangu  
kutoka kwa Mungu  
kuhusu hali ya dhambi ya mwovu.  
Hakuna hofu ya Mungu  
mbele ya macho yake.   
 2 Kwa kuwa machoni pake mwenyewe hujisifu mno  
hata hawezi kugundua au kuichukia dhambi yake.   
 3 Maneno ya kinywa chake ni maovu na ya udanganyifu,  
ameacha kuwa mwenye hekima au kutenda mema.   
 4 Hata kitandani mwake hupanga hila mbaya,  
hujitia katika njia ya dhambi  
na hakatai lililo baya.   
 5 Upendo wako, Ee Mwenyezi Mungu, unafika hadi mbinguni,  
uaminifu wako hadi kwenye anga.   
 6 Haki yako ni kama milima mikubwa,  
hukumu zako ni kama kilindi kikuu.  
Ee Mwenyezi Mungu, wewe huwahifadhi  
mwanadamu na mnyama.   
 7 Upendo wako usiokoma  
ni wa thamani mno!  
Watu wakuu na wadogo  
hujificha uvulini wa mabawa yako.   
 8 Wanajifurahisha katika wingi ulio nyumbani mwako,  
nawe utawanywesha katika mto wa furaha zako.   
 9 Kuwa pamoja nawe ni kijito cha uzima,  
katika nuru yako twaona nuru.   
 10 Dumisha upendo wako kwa wale wanaokujua wewe,  
haki yako kwa wale walio wanyofu wa moyo.   
 11 Mguu wa mwenye kiburi usije dhidi yangu,  
wala mkono wa mwovu usinifukuze.   
 12 Tazama jinsi watenda maovu walivyoanguka:  
wametupwa chini, hawawezi kuinuka!