*Zaburi hii imetungwa kila beti likianzia na herufi ya alfabeti ya Kiebrania zikifuatana tangu Aleph (A) hadi Taw (T); zote ni 22.
Zaburi 37
Mwisho wa mwovu na urithi wa mwenye haki
Zaburi ya Daudi.
Usisumbuke kwa ajili ya watendao maovu,
wala usiwaonee wivu watendao mabaya,
kwa maana watanyauka upesi kama majani,
watakufa upesi kama mimea ya kijani.
 
Mtumaini Mwenyezi Mungu na utende yaliyo mema.
Kaa katika nchi ukafurahie malisho salama.
Jifurahishe katika Mwenyezi Mungu
naye atakupa haja za moyo wako.
 
Mkabidhi Mwenyezi Mungu njia yako,
mtumaini yeye, naye atatenda hili:
Yeye atafanya haki yako ing’ae kama mapambazuko,
na hukumu ya shauri lako kama jua la adhuhuri.
 
Tulia mbele za Mwenyezi Mungu
na umngojee kwa uvumilivu;
usisumbuke watu wanapofanikiwa katika njia zao,
wanapotekeleza mipango yao miovu.
 
Epuka hasira na uache ghadhabu;
usihangaike: itakuongoza tu kutenda uovu.
Kwa maana waovu watakatiliwa mbali,
bali wale wanaomtumaini Mwenyezi Mungu watairithi nchi.
 
10 Bado kitambo kidogo, nao waovu hawataonekana,
ingawa utawatafuta, hawataonekana.
11 Bali wanyenyekevu watairithi nchi
na wafurahie amani tele.
 
12 Waovu hula njama dhidi ya wenye haki
na kuwasagia meno,
13 bali Bwana huwacheka waovu,
kwa sababu anajua siku yao inakuja.
 
14 Waovu hufuta upanga
na kupinda upinde,
ili wawaangushe maskini na wahitaji,
kuwaua wale ambao njia zao ni nyofu.
15 Lakini panga zao zitachoma mioyo yao wenyewe,
na pinde zao zitavunjwa.
 
16 Bora kidogo walicho nacho wenye haki
kuliko wingi wa mali ya waovu wengi;
17 kwa maana nguvu za waovu zitavunjwa,
lakini Mwenyezi Mungu humtegemeza mwenye haki.
 
18 Mwenyezi Mungu anazifahamu siku za wanyofu,
na urithi wao utadumu milele.
19 Siku za maafa hawatanyauka,
siku za njaa watafurahia wingi wa vitu.
 
20 Lakini waovu wataangamia:
Adui za Mwenyezi Mungu watakuwa
kama uzuri wa mashamba,
watatoweka,
watatoweka kama moshi.
 
21 Waovu hukopa na hawalipi,
bali wenye haki hutoa kwa ukarimu.
22 Wale wanaobarikiwa na Mwenyezi Mungu watairithi nchi,
bali wale anaowalaani watakatiliwa mbali.
 
23 Kama Mwenyezi Mungu akipendezwa na njia ya mtu,
yeye huimarisha hatua zake,
24 ajapojikwaa, hataanguka,
kwa maana Mwenyezi Mungu
humtegemeza kwa mkono wake.
 
25 Nilikuwa kijana na sasa ni mzee,
lakini sijaona kamwe wenye haki wameachwa
au watoto wao wakiombaomba chakula.
26 Wakati wote ni wakarimu na hukopesha bila masharti.
Watoto wao watabarikiwa.
 
27 Acha ubaya na utende wema,
nawe utaishi katika nchi milele.
28 Kwa kuwa Mwenyezi Mungu huwapenda wenye haki
naye hatawaacha waaminifu wake.
 
Watalindwa milele,
lakini uzao wa waovu utakatiliwa mbali.
29 Wenye haki watairithi nchi,
na kuishi humo milele.
 
30 Kinywa cha mwenye haki hutamka hekima,
nao ulimi wake huzungumza lililo haki.
31 Torati ya Mungu wake imo moyoni mwake;
nyayo zake hazitelezi.
 
32 Watu waovu huvizia wenye haki,
wakitafuta kuwaua;
33 lakini Mwenyezi Mungu hatawaacha mikononi mwao
wala hatawaacha wahukumiwe
kuwa wakosa wanaposhtakiwa.
 
34 Mngojee Mwenyezi Mungu,
na uishike njia yake.
Naye atakutukuza uirithi nchi,
waovu watakapokatiliwa mbali,
utaliona hilo.
 
35 Nimemwona mtu mwovu na mkatili akistawi
kama mwerezi wa Lebanoni,
36 lakini alitoweka upesi na hakuonekana,
ingawa nilimtafuta, hakupatikana.
 
37 Watafakari watu wasio na hatia,
wachunguze watu wakamilifu,
kuna mafanikio kwa mtu apendaye amani.
38 Lakini watenda dhambi wote wataangamizwa,
mafanikio yao yatakatiliwa mbali.
 
39 Wokovu wa wenye haki hutoka kwa Mwenyezi Mungu,
yeye ni ngome yao wakati wa shida.
40 Mwenyezi Mungu huwasaidia na kuwaokoa,
huwaokoa kutoka kwa waovu na kuwahifadhi,
kwa maana wanamkimbilia.

*^ Zaburi hii imetungwa kila beti likianzia na herufi ya alfabeti ya Kiebrania zikifuatana tangu Aleph (A) hadi Taw (T); zote ni 22.