Zaburi 38
Maombi ya mtu anayeteseka
Zaburi ya Daudi. Maombi.
1 Ee Mwenyezi Mungu, usinikemee katika hasira yako,
wala kuniadhibu katika ghadhabu yako.
2 Kwa kuwa mishale yako imenichoma,
na mkono wako umenipiga.
3 Hakuna afya mwilini mwangu
kwa sababu ya ghadhabu yako,
mifupa yangu haina uzima
kwa sababu ya dhambi zangu.
4 Maovu yangu yamenifunika
kama mzigo mzito mno.
5 Majeraha yangu yameoza na yananuka,
kwa sababu ya upumbavu wa dhambi zangu.
6 Nimeinamishwa chini na kushushwa sana,
mchana kutwa nazunguka nikiomboleza.
7 Viuno vyangu vimejaa maumivu yaunguzayo,
hakuna afya mwilini mwangu.
8 Nimedhoofika na kupondwa kabisa,
nasononeka kwa maumivu makuu ya moyoni.
9 Ee Bwana, yote ninayoyaonea shauku
yako wazi mbele zako,
kutamani kwangu sana
hakufichiki mbele zako.
10 Moyo wangu unapigapiga,
nguvu zangu zimeniishia;
hata macho yangu yametiwa giza.
11 Rafiki na wenzangu wananikwepa
kwa sababu ya majeraha yangu;
majirani wangu wanakaa mbali nami.
12 Wale wanaotafuta uhai wangu
wanatega mitego yao,
wale ambao wangetaka kunidhuru
huongea kuhusu maangamizi yangu;
hupanga hila mchana kutwa.
13 Mimi ni kama kiziwi, asiyeweza kusikia,
ni kama bubu, asiyeweza kufungua kinywa chake;
14 nimekuwa kama mtu asiyesikia,
ambaye kinywa chake hakiwezi kutoa jibu.
15 Ee Mwenyezi Mungu, ninakungojea wewe,
Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, utajibu.
16 Kwa kuwa nilisema, “Usiwaache wafurahie,
wala wajitukuze juu yangu
mguu wangu unapoteleza.”
17 Kwa maana ninakaribia kuanguka,
na maumivu yangu yananiandama siku zote.
18 Naungama uovu wangu,
ninataabishwa na dhambi yangu.
19 Wengi wamekua adui zangu bila sababu;
wale wanaonichukia bure ni wengi.
20 Wanaolipa wema wangu kwa maovu
hunisingizia ninapofuata lililo jema.
21 Ee Mwenyezi Mungu, usiniache,
usiwe mbali nami, Ee Mungu wangu.
22 Ee Bwana Mwokozi wangu,
uje upesi kunisaidia.