Zaburi 41
Maombi ya mtu mgonjwa
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi.
1 Heri mtu yule anayemjali mnyonge,
Mwenyezi Mungu atamwokoa wakati wa shida.
2 Mwenyezi Mungu atamlinda na kuyahifadhi maisha yake,
atambariki katika nchi
na hatamwacha katika tamaa ya adui zake.
3 Mwenyezi Mungu atamtegemeza akiwa mgonjwa kitandani,
na atamwinua kutoka kitandani mwake.
4 Nilisema, “Ee Mwenyezi Mungu nihurumie,
niponye, maana nimekutenda dhambi wewe.”
5 Adui zangu wanasema kwa hila,
“Lini atakufa, na jina lake litokomee kabisa.”
6 Kila anapokuja mtu kunitazama,
huzungumza uongo,
huku moyo wake ukikusanya masingizio;
kisha huondoka na kuyasambaza.
7 Adui zangu wote hunong’onezana dhidi yangu,
hao huniwazia mabaya sana, wakisema,
8 “Ugonjwa mbaya sana umempata,
kamwe hatainuka tena kitandani mwake.”
9 Hata rafiki yangu wa karibu niliyemwamini,
yule aliyekula chakula changu
ameniinulia kisigino chake.
10 Lakini wewe, Ee Mwenyezi Mungu, nihurumie,
ukaniinue tena, ili niweze kuwalipiza kisasi.
11 Najua kwamba wapendezwa nami,
kwa kuwa adui yangu hanishindi.
12 Katika uadilifu wangu unanitegemeza
na kuniweka kwenye uwepo wako milele.
13 Mtukuzeni Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli,
tangu milele na hata milele.
Amen na Amen.