Kitabu cha Pili  
 42
(Zaburi 42–72)  
Maombi ya mtu aliye uhamishoni 
 Kwa mwimbishaji. Utenzi wa wana wa Kora. 
  1 Kama ayala anavyoonea shauku vijito vya maji,  
ndivyo nafsi yangu inavyokuonea shauku, Ee Mungu.   
 2 Nafsi yangu inamwonea Mungu kiu, Mungu aliye hai.  
Ni lini nitaweza kwenda kukutana na Mungu?   
 3 Machozi yangu yamekuwa chakula changu  
usiku na mchana,  
huku watu wakiniambia mchana kutwa,  
“Yuko wapi Mungu wako?”   
 4 Mambo haya nayakumbuka  
ninapoimimina nafsi yangu:  
Jinsi nilivyokuwa nikienda na umati wa watu,  
nikiongoza maandamano kuelekea kwenye nyumba ya Mungu,  
kwa kelele za shangwe na za shukrani  
katikati ya umati wa watu waliosherehekea.   
 5 Ee nafsi yangu, kwa nini unasononeka?  
Kwa nini unafadhaika hivyo ndani yangu?  
Weka tumaini lako kwa Mungu,  
kwa kuwa bado nitamsifu,  
Mwokozi wangu na Mungu wangu.   
 6 Nafsi yangu inasononeka ndani yangu;  
kwa hiyo nitakukumbuka  
kutoka nchi ya Yordani,  
katika vilele vya Hermoni,  
kutoka Mlima Mizari.   
 7 Kilindi huita kilindi,  
katika ngurumo za maporomoko ya maji yako;  
mawimbi yako yote pamoja na viwimbi  
vimepita juu yangu.   
 8 Mwenyezi Mungu huelekeza upendo wake mchana,  
wimbo wake uko nami usiku:  
maombi kwa Mungu wa uzima wangu.   
 9 Ninamwambia Mungu Mwamba wangu,  
“Kwa nini umenisahau?  
Kwa nini niendelee kuomboleza,  
nikiteswa na adui?”   
 10 Mifupa yangu inateseka kwa maumivu makali  
adui zangu wanaponidhihaki,  
wakiniambia mchana kutwa,  
“Yuko wapi Mungu wako?”   
 11 Ee nafsi yangu, kwa nini unasononeka?  
Kwa nini unafadhaika hivyo ndani yangu?  
Weka tumaini lako kwa Mungu,  
kwa kuwa bado nitamsifu,  
Mwokozi wangu na Mungu wangu.