Zaburi 43
Maombi ya mtu aliye uhamishoni yanaendelea
1 Ee Mungu unihukumu,
nitetee dhidi ya taifa lisilomcha Mungu,
niokoe na watu wadanganyifu na waovu.
2 Wewe ni Mungu ngome yangu.
Kwa nini umenikataa?
Kwa nini niendelee kuomboleza,
nikidhulumiwa na adui?
3 Tuma hima nuru yako na kweli yako viniongoze;
na vinilete hadi mlima wako mtakatifu,
mahali unapoishi.
4 Ndipo nitaenda madhabahuni pa Mungu,
kwa Mungu, furaha yangu na shangwe yangu.
Nitakusifu kwa kinubi,
Ee Mungu, Mungu wangu.
5 Ee nafsi yangu, kwa nini unasononeka?
Kwa nini unafadhaika hivyo ndani yangu?
Weka tumaini lako kwa Mungu,
kwa sababu bado nitamsifu
Mwokozi wangu na Mungu wangu.