Zaburi 45
Wimbo wa arusi ya kifalme 
 Kwa mwimbishaji. Mtindo wa utenzi wa “Yungiyungi”. Utenzi wa wana wa Kora. Wimbo wa arusi. 
  1 Moyo wangu umesisimuliwa na jambo jema  
ninapomsimulia mfalme mabeti yangu;  
ulimi wangu ni kalamu ya mwandishi stadi.   
 2 Wewe ni bora kuliko watu wengine wote  
na midomo yako imepakwa neema,  
kwa kuwa Mungu amekubariki milele.   
 3 Jifunge upanga wako pajani mwako, ee mwenye nguvu,  
jivike fahari na utukufu.   
 4 Katika fahari yako, songa mbele kwa ushindi,  
kwa ajili ya kweli, unyenyekevu na haki,  
mkono wako wa kuume na uoneshe matendo ya kutisha.   
 5 Mishale yako mikali na ichome mioyo ya adui za mfalme,  
mataifa na yaanguke chini ya nyayo zako.   
 6 Ee Mungu, kiti chako cha enzi  
kitadumu milele na milele,  
fimbo ya utawala wa haki  
itakuwa fimbo ya utawala wa ufalme wako.   
 7 Unaipenda haki na kuchukia uovu;  
kwa hiyo Mungu, Mungu wako,  
amekuweka juu ya wenzako,  
kwa kukupaka mafuta ya furaha.   
 8 Mavazi yako yote yana harufu nzuri  
ya manemane, udi na mdalasini;  
kutoka majumba ya kifalme  
yaliyopambwa kwa pembe za ndovu,  
sauti za vinanda vya nyuzi  
zinakufanya ufurahi.   
 9 Binti za wafalme ni miongoni mwa wanawake wako waheshimiwa;  
kuume kwako yupo bibi arusi malkia aliyevaa dhahabu ya Ofiri.   
 10 Sikiliza, ewe binti, fikiri na utege sikio:  
Sahau watu wako na nyumba ya baba yako.   
 11 Mfalme ameshangazwa na uzuri wako;  
mheshimu, kwa kuwa yeye ni bwana wako.   
 12 Binti Tiro atakuletea zawadi,  
watu wenye utajiri watatafuta upendeleo wako.   
 13 Ufahari wote una binti mfalme katika chumba chake;  
vazi lake limefumwa kwa nyuzi za dhahabu.   
 14 Anaongozwa kwa mfalme,  
akiwa amevalia mavazi yaliyotariziwa,  
mabikira wenzake wanamfuata  
na wanaletwa kwako.   
 15 Wanaingizwa ndani kwa shangwe na furaha,  
na kuingia katika jumba la mfalme.   
 16 Wana wenu watachukua nafasi za baba zenu,  
mtawafanya wakuu katika nchi yote.   
 17 Nitadumisha kumbukumbu lako katika vizazi vyote,  
kwa hiyo mataifa watakusifu milele na milele.