Zaburi 46
Mwenyezi Mungu yuko pamoja nasi
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya wana wa Kora. Mtindo wa alamothi.
Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu,
msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso.
Kwa hiyo hatutaogopa, hata kama dunia ikiondolewa,
na milima ianguke kilindini cha bahari,
hata maji yake yakinguruma na kuumuka,
na milima itetemeke kwa mawimbi yake.
 
Kuna mto ambao vijito vyake vinaufurahisha mji wa Mungu,
mahali patakatifu ambako Aliye Juu Sana anaishi.
Mungu yuko katikati yake, hautaanguka,
Mungu atausaidia asubuhi na mapema.
Mataifa yanafanya ghasia, falme zinaanguka,
yeye hupaza sauti yake, dunia ikayeyuka.
 
Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni
yu pamoja nasi;
Mungu wa Yakobo ni ngome yetu.
 
Njooni mkaone kazi za Mwenyezi Mungu
jinsi alivyofanya ukiwa katika nchi.
Anakomesha vita hata miisho ya dunia,
anakata upinde na kuvunjavunja mkuki,
anateketeza ngao kwa moto.
10 “Tulieni, mjue kwamba mimi ndimi Mungu;
nitatukuzwa katikati ya mataifa,
nitatukuzwa katika dunia.”
 
11 Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni
yu pamoja nasi;
Mungu wa Yakobo ni ngome yetu.