Zaburi 47
Mtawala mwenye enzi yote
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya wana wa Kora.
Pigeni makofi, enyi mataifa yote,
mpigieni Mungu kelele za shangwe!
Jinsi gani alivyo wa kutisha, Mwenyezi Mungu Aliye Juu Sana,
Mfalme mkuu juu ya dunia yote!
Ametiisha mataifa chini yetu,
watu wengi chini ya miguu yetu.
Alituchagulia urithi wetu,
fahari ya Yakobo, aliyempenda.
 
Mungu amepaa kwa kelele za shangwe,
Mwenyezi Mungu kwa sauti za tarumbeta.
Mwimbieni Mungu sifa, imbeni sifa,
mwimbieni sifa Mfalme wetu, imbeni sifa.
 
Kwa kuwa Mungu ni mfalme wa dunia yote,
mwimbieni zaburi za sifa.
Mungu anayatawala mataifa,
Mungu ameketi kwenye kiti chake cha enzi kitakatifu.
Wakuu wa mataifa wanakusanyika
kama watu wa Mungu wa Ibrahimu,
kwa kuwa wafalme wa dunia ni mali ya Mungu;
yeye ametukuka sana.