Zaburi 48
Sayuni, mji wa Mwenyezi Mungu
Wimbo. Zaburi ya wana wa Kora.
Mwenyezi Mungu ni mkuu, anayestahili kusifiwa sana,
katika mji wa Mungu wetu,
mlima wake mtakatifu.
Ni mzuri katika kuinuka juu kwake,
furaha ya dunia yote.
Kama vilele vya juu vya Safoni*au mlima mtakatifu au upande wa kaskazini ni Mlima Sayuni,
mji wa Mfalme Mkuu.
Mungu yuko katika ngome zake;
amejionesha mwenyewe kuwa ngome yake.
 
Wafalme walipounganisha nguvu,
waliposonga mbele pamoja,
walimwona, wakashangaa,
wakakimbia kwa hofu.
Kutetemeka kuliwashika huko,
maumivu kama ya mwanamke
mwenye uchungu wa kuzaa.
Uliwaangamiza kama meli za Tarshishi
zilizovunjwa na upepo wa mashariki.
 
Kama tulivyokuwa tumesikia,
ndivyo tulivyoona
katika mji wa Mwenyezi Mungu,
Mungu wa majeshi ya mbinguni,
katika mji wa Mungu wetu:
Mungu ataufanya uwe salama milele.
 
Ee Mungu, hekaluni mwako
tunatafakari upendo wako usiokoma.
10 Ee Mungu, kama jina lako lilivyo,
sifa zako zinafika hadi miisho ya dunia,
mkono wako wa kuume umejazwa na haki.
11 Mlima Sayuni unashangilia,
vijiji vya Yuda vinafurahi
kwa sababu ya hukumu zako.
 
12 Tembeeni katika Sayuni,
uzungukeni mji,
hesabuni minara yake;
13 yatafakarini vyema maboma yake,
angalieni ngome zake,
ili mpate kusimulia habari zake
kwa kizazi kijacho.
14 Kwa kuwa huyu Mungu ni Mungu wetu milele na milele;
atakuwa kiongozi wetu hata mwisho.

*Zaburi 48:2 au mlima mtakatifu au upande wa kaskazini