Zaburi 52
Hukumu ya Mwenyezi Mungu 
 Kwa mwimbishaji. Utenzi wa Daudi. Baada ya Doegi, Mwedomu kumwendea Sauli na kumjulisha kuwa: “Daudi ameenda nyumbani mwa Ahimeleki.” 
  1 Ewe jitu, mbona unajivunia ubaya?  
Kwa nini unajivuna mchana kutwa,  
wewe ambaye ni fedheha mbele za Mungu?   
 2 Ulimi wako hupanga mashauri mabaya ya maangamizi.  
Ni kama wembe mkali, ninyi mnaofanya hila.   
 3 Unapenda mabaya kuliko mema,  
uongo kuliko kusema kweli.   
 4 Unapenda kila neno lenye kudhuru,  
ewe ulimi wenye hila!   
 5 Hakika Mungu atakushusha chini  
kwa maangamizi ya milele:  
atakunyakua na kukuondoa kwa nguvu  
kutoka hema lako,  
atakung’oa kutoka nchi ya walio hai.   
 6 Wenye haki wataona na kuogopa;  
watamcheka, wakisema,   
 7 “Huyu ni yule mtu ambaye  
hakumfanya Mungu kuwa ngome yake,  
bali alitumainia wingi wa utajiri wake,  
na akawa hodari kwa kuwaangamiza wengine!”   
Neema ya Mwenyezi Mungu 
  8 Lakini mimi ni kama mti wa mzeituni  
unaostawi katika nyumba ya Mungu,  
nautegemea upendo wa Mungu usiokoma  
milele na milele.   
 9 Nitakusifu milele kwa yale uliyoyatenda,  
nitatumaini jina lako, kwa kuwa jina lako ni jema.  
Nitakusifu mbele ya watakatifu wako.