Zaburi 53
Uovu wa wanadamu
(Zaburi 14)
Kwa mwimbishaji. Mtindo wa mahalathi. Utenzi wa Daudi.
1 Mpumbavu anasema moyoni mwake,
“Hakuna Mungu.”
Wameharibika, na njia zao ni za uovu kabisa,
hakuna hata mmoja atendaye mema.
2 Mungu anawachungulia wanadamu chini
kutoka mbinguni
aone kama wako wenye akili,
wowote wanaomtafuta Mungu.
3 Kila mmoja amegeukia mbali,
wameharibika wote pamoja,
hakuna atendaye mema.
Naam, hakuna hata mmoja!
4 Je, watendao maovu kamwe hawatajifunza:
wale ambao huwala watu wangu
kama watu walavyo mkate,
hao ambao hawamwiti Mungu?
5 Hapo waliingiwa na hofu kuu,
ambapo hapakuwa na hofu.
Mungu alitawanya mifupa ya wale waliokushambulia;
uliwaaibisha, kwa sababu Mungu aliwadharau.
6 Laiti wokovu wa Israeli ungekuja kutoka Sayuni!
Mungu anaporejesha wafungwa wa watu wake,
Yakobo na ashangilie, Israeli na afurahi!