Zaburi 61
Kuomba ulinzi
Kwa mwimbishaji. Kwa ala za nyuzi za uimbaji. Zaburi ya Daudi.
Ee Mungu, sikia kilio changu,
usikilize maombi yangu.
 
Kutoka miisho ya dunia ninakuita,
ninakuita huku moyo wangu unadhoofika;
uniongoze kwenye mwamba
ulio juu kuniliko.
Kwa kuwa umekuwa kimbilio langu,
ngome imara dhidi ya adui.
 
Natamani kukaa kwenye hema lako milele,
na kukimbilia chini ya uvuli wa mabawa yako.
Ee Mungu, kwa kuwa umesikia nadhiri zangu,
umenipa urithi wa wale wanaoliogopa jina lako.
 
Mwongezee mfalme siku za maisha yake,
miaka yake kwa vizazi vingi.
Mtawaze mbele za Mungu milele;
amuru upendo wako na uaminifu wako vimlinde.
 
Ndipo daima nitaliimbia sifa jina lako
na kuzitimiza nadhiri zangu siku baada ya siku.