Zaburi 62
Mwenyezi Mungu kimbilio la pekee
Kwa mwimbishaji. Mtindo wa Yeduthuni. Zaburi ya Daudi.
Nafsi yangu inapata pumziko kwa Mungu peke yake;
wokovu wangu watoka kwake.
Yeye peke yake ndiye mwamba wangu na wokovu wangu;
yeye ni ngome yangu, sitatikisika kamwe.
 
Mtanishambulia hadi lini?
Je, ninyi nyote mtanitupa chini:
Mimi niliye kama ukuta ulioinama,
kama uzio unaotikisika?
Walikusudia kikamilifu kumwangusha
toka mahali pake pa fahari;
wanafurahia uongo.
Kwa vinywa vyao hubariki,
lakini ndani ya mioyo yao hulaani.
 
Ee nafsi yangu, upumzike, kwa Mungu peke yake,
tumaini langu latoka kwake.
Yeye peke yake ndiye mwamba wangu na wokovu wangu;
ndiye ngome yangu, sitatikisika.
Wokovu wangu na heshima yangu viko kwa Mungu,
ndiye mwamba wangu wenye nguvu
na kimbilio langu.
Enyi watu, mtumainini yeye wakati wote,
miminieni mioyo yenu kwake,
kwa kuwa Mungu ni kimbilio letu.
 
Binadamu wa ngazi ya chini ni pumzi tu,
nao wa ngazi ya juu ni uongo tu;
wakipimwa kwenye mizani, si chochote;
wote kwa pamoja ni pumzi tu.
10 Usitumainie udhalimu,
wala ujivune kwa vitu vya wizi;
ingawa utajiri wako utaongezeka,
usiuweke moyoni mwako.
 
11 Jambo moja Mungu amelisema,
mambo mawili nimeyasikia:
kwamba, Ee Mungu,
wewe una nguvu,
12 na kwamba, Ee Bwana,
wewe ni mwenye upendo.
Hakika utampa kila mtu thawabu
kwa kadiri ya alivyotenda.