Zaburi 63
Shauku kwa ajili ya uwepo wa Mwenyezi Mungu
Zaburi ya Daudi. Alipokuwa katika Jangwa la Yuda.
1 Ee Mungu, wewe ni Mungu wangu,
nakutafuta kwa moyo wote;
nafsi yangu inakuonea kiu,
mwili wangu unakuonea wewe shauku,
katika nchi kame na iliyochoka,
mahali pasipo maji.
2 Nimekuona katika mahali patakatifu
na kuuona uwezo wako na utukufu wako.
3 Kwa sababu upendo wako ni bora kuliko uhai,
midomo yangu itakuadhimisha.
4 Nitakusifu siku zote za maisha yangu,
na kwa jina lako nitainua mikono yangu.
5 Nafsi yangu itatoshelezwa,
kama kushiba vyakula vizuri;
kwa midomo iimbayo
kinywa changu kitakusifu wewe.
6 Kitandani mwangu ninakukumbuka wewe;
ninakuwaza makesha yote ya usiku.
7 Kwa sababu wewe ndiwe msaada wangu,
chini ya uvuli wa mabawa yako naimba.
8 Nafsi yangu inaambatana nawe,
mkono wako wa kuume hunishika.
9 Wale wanaotafuta uhai wangu wataangamizwa;
wataenda chini kwenye vilindi vya dunia.
10 Watatolewa wafe kwa upanga,
nao watakuwa chakula cha mbweha.
11 Bali mfalme atafurahi katika Mungu,
wale wote waapao kwa jina la Mungu watamsifu,
bali vinywa vya waongo vitanyamazishwa.