Zaburi 68
Wimbo wa taifa wa shangwe kwa ushindi
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. Wimbo.
Mungu na ainuke, watesi wake watawanyike,
adui zake na wakimbie mbele zake.
Kama moshi unavyopeperushwa na upepo,
vivyo hivyo uwapeperushe mbali,
kama nta inavyoyeyuka kwenye moto,
vivyo hivyo waovu na waangamie mbele za Mungu.
Bali wenye haki na wafurahi,
washangilie mbele za Mungu,
wafurahi na kushangilia.
 
Mwimbieni Mungu, liimbieni sifa jina lake,
mtukuzeni yeye anayepita juu ya mawingu:
jina lake ni Mwenyezi Mungu,
furahini mbele zake.
Baba wa yatima, mtetezi wa wajane,
ni Mungu katika makao yake matakatifu.
Mungu huwaweka wapweke katika jamaa,
huwaongoza wafungwa wakiimba,
bali waasi huishi katika nchi kame.
 
Ee Mungu, ulipowatangulia watu wako,
ulipopita nyikani,
dunia ilitikisika,
mbingu zikanyesha mvua,
mbele za Mungu, Yule wa Sinai,
mbele za Mungu, Mungu wa Israeli.
Ee Mungu, ulinyesha mvua nyingi
na kuiburudisha ardhi iliyokuwa imechoka.
10 Ee Mungu, watu wako waliishi huko,
nawe kwa wingi wa utajiri wako
uliwapa maskini mahitaji yao.
 
11 Bwana analitoa neno,
wanawake wanaolitangaza
neno hilo ni kundi kubwa:
12 “Wafalme na majeshi walikimbia upesi,
wanawake waliobaki nyumbani waligawana nyara.
13 Hata unapolala kati ya mioto ya kambini,
mabawa ya njiwa wangu yamefunikwa kwa fedha,
manyoya yake kwa dhahabu inayong’aa.”
14 Mwenyezi*Mwenyezi hapa ina maana ya Shaddai kwa Kiebrania. alipowatawanya wafalme katika nchi,
ilikuwa kama theluji iliyoanguka juu ya Mlima Salmoni.
 
15 Milima ya Bashani ni milima iliyotukuka,
milima ya Bashani ina vilele vilivyochongoka.
16 Enyi milima yenye vilele vilivyochongoka,
kwa nini mnakazia macho kwa wivu,
katika mlima Mungu anaochagua kutawala,
ambako Mwenyezi Mungu mwenyewe ataishi milele?
17 Magari ya vita ya Mungu ni makumi ya maelfu,
na maelfu ya maelfu;
Bwana amekuja kutoka Sinai
hadi katika patakatifu pake.
18 Ulipopanda juu, uliteka mateka,
ukapokea vipawa kutoka kwa wanadamu,
hata kutoka kwa wale walioasi,
ili wewe, Ee Bwana Mwenyezi Mungu, upate kuishi huko.
 
19 Ahimidiwe Bwana, Mungu Mwokozi wetu,
ambaye siku kwa siku hutuchukulia mizigo yetu.
20 Mungu wetu ni Mungu anayeokoa,
Bwana Mungu Mwenyezi hutuokoa na kifo.
 
21 Hakika Mungu ataponda vichwa vya adui zake,
vichwa vya hao wanaoenda katika njia za dhambi.
22 Bwana alisema, “Nitawarudisha kutoka Bashani;
nitawarudisha kutoka vilindi vya bahari,
23 ili uweze kuchovya miguu yako katika damu ya adui zako,
huku ndimi za mbwa wako zikiwa na fungu lake.”
 
24 Ee Mungu, maandamano yako yameonekana,
maandamano ya Mungu wangu, Mfalme wangu,
yakielekea patakatifu pake.
25 Mbele wako waimbaji, baada yao wapiga vinanda,
pamoja nao wako wanawali wakipiga matari.
26 Msifuni Mungu katika kusanyiko kubwa,
msifuni Mwenyezi Mungu katika kusanyiko la Israeli.
27 Liko kabila dogo la Benyamini likiwaongoza,
wakifuatwa na kundi kubwa la watawala wa Yuda,
hatimaye watawala wa Zabuloni na Naftali.
 
28 Ee Mungu, amuru uwezo wako,
Ee Mungu tuoneshe nguvu zako,
kama ulivyofanya hapo awali.
29 Kwa sababu ya Hekalu lako Yerusalemu
wafalme watakuletea zawadi.
30 Mkemee mnyama aliye kwenye matete,
kundi la mafahali kati ya ndama za mataifa.
Na walete minara ya madini ya fedha wakinyenyekea.
Tawanya mataifa yapendayo vita.
31 Wajumbe watakuja kutoka Misri;
Kushi atajisalimisha kwa Mungu.
 
32 Mwimbieni Mungu, enyi falme za dunia,
mwimbieni Bwana sifa,
33 mwimbieni sifa yeye apandaye mbingu za kale zilizo juu,
yeye angurumaye kwa sauti kuu.
34 Tangazeni uwezo wa Mungu,
ambaye fahari yake iko juu ya Israeli,
ambaye uwezo wake uko katika anga.
35 Ee Mungu, wewe unatisha katika mahali patakatifu pako,
Mungu wa Israeli huwapa watu wake uwezo na nguvu.
 
Ahimidiwe Mungu!

*Zaburi 68:14 Mwenyezi hapa ina maana ya Shaddai kwa Kiebrania.