Zaburi 74
Maombi kwa ajili ya taifa
Utenzi wa Asafu.
1 Ee Mungu, mbona umetukataa milele?
Mbona hasira yako inatoka moshi
juu ya kondoo wa malisho yako?
2 Kumbuka watu uliowanunua zamani,
kabila la urithi wako, ambao uliwakomboa:
Mlima Sayuni, ambamo uliishi.
3 Geuza hatua zako kuelekea magofu haya ya kudumu,
uharibifu wote huu ambao adui ameuleta pale patakatifu.
4 Adui zako wamenguruma pale ulipokutana nasi,
wanaweka bendera zao kama alama.
5 Walifanya kama watu wanaotumia mashoka
kukata kichaka cha miti.
6 Walivunjavunja milango yote iliyonakshiwa
kwa mashoka na vishoka vyao.
7 Waliteketeza kabisa mahali pako patakatifu,
wakayanajisi makao ya Jina lako.
8 Walisema mioyoni mwao,
“Tutawaponda kabisa!”
Walichoma kila mahali Mungu
alipoabudiwa katika nchi.
9 Hatukupewa ishara za miujiza;
hakuna manabii waliobaki,
hakuna yeyote kati yetu ajuaye
hali hii itachukua muda gani.
10 Ee Mungu, mtesi atakudhihaki hadi lini?
Je, adui watalitukana jina lako milele?
11 Kwa nini unazuia mkono wako,
mkono wako wa kuume?
Uutoe kutoka makunjo ya vazi lako
na uwaangamize!
12 Lakini wewe, Ee Mungu, ni mfalme wangu tangu zamani,
unaleta wokovu duniani.
13 Ni wewe uliyeigawanya bahari kwa uweza wako;
ulivunja vichwa vya mnyama mkubwa wa baharini.
14 Ni wewe uliyeponda vichwa vya Lewiathani*Lewiathani ni mnyama mkubwa wa baharini mwenye magamba anayefanana na joka kubwa, mwenye umbo la kutisha, asiyeweza kuvuliwa.,
nawe ukamtoa kama chakula kwa viumbe vya jangwani.
15 Ni wewe uliyefungua chemchemi na vijito,
ulikausha mito iliyokuwa ikitiririka daima.
16 Mchana ni wako, na usiku ni wako pia;
uliziweka jua na mwezi.
17 Ni wewe uliyeiweka mipaka yote ya dunia,
ulifanya kiangazi na masika.
18 Ee Mwenyezi Mungu, kumbuka jinsi mtesi alivyokudhihaki,
jinsi watu wapumbavu walivyolitukana jina lako.
19 Usiukabidhi uhai wa njiwa wako kwa wanyama mwitu;
usisahau kabisa uhai wa watu wako wanaoteseka milele.
20 Likumbuke agano lako,
maana mara kwa mara mambo ya jeuri
yamejaa katika sehemu za giza nchini.
21 Usiruhusu waliodhulumiwa warudi nyuma kwa aibu;
maskini na wahitaji hebu walisifu jina lako.
22 Inuka, Ee Mungu, ujitetee;
kumbuka jinsi wapumbavu
wanavyokudhihaki mchana kutwa.
23 Usipuuze makelele ya watesi wako,
ghasia za adui zako, zinazoinuka mfululizo.
*Zaburi 74:14 Lewiathani ni mnyama mkubwa wa baharini mwenye magamba anayefanana na joka kubwa, mwenye umbo la kutisha, asiyeweza kuvuliwa.