Zaburi 75
Mwenyezi Mungu ni mwamuzi 
 Kwa mwimbishaji. Mtindo wa “Usiharibu”. Zaburi ya Asafu. Wimbo. 
  1 Ee Mungu, tunakushukuru,  
tunakushukuru wewe,  
kwa kuwa jina lako li karibu;  
watu husimulia matendo yako ya ajabu.   
 2 Unasema, “Ninachagua wakati maalum;  
ni mimi nihukumuye kwa haki.   
 3 Dunia inapotetemeka na watu wake wote,  
ni mimi ninayezishikilia nguzo zake imara.   
 4 Kwa wale wenye majivuno ninasema,  
‘Msijisifu tena,’  
kwa wale waovu, ‘Msiinue pembe zenu.   
 5 Msiinue pembe zenu dhidi ya mbingu;  
msiseme kwa kiburi.’ ”   
 6 Hakuna yeyote atokaye mashariki wala magharibi  
au kutoka jangwani awezaye kumkweza mwanadamu.   
 7 Bali Mungu ndiye ahukumuye:  
Humshusha huyu na kumkweza mwingine.   
 8 Mkononi mwa Mwenyezi Mungu kuna kikombe  
kilichojaa mvinyo unaotoka povu  
uliochanganywa na vikolezo;  
huumimina, nao waovu wote wa dunia  
hunywa hata tone la mwisho.   
 9 Bali mimi, nitatangaza hili milele;  
nitaimba sifa kwa Mungu wa Yakobo.   
 10 Nitazikatilia mbali pembe za waovu wote,  
bali pembe za wenye haki zitainuliwa juu.