Zaburi 81
Wimbo wa sikukuu
Kwa mwimbishaji. Mtindo wa gitithi. Zaburi ya Asafu.
1 Mwimbieni kwa furaha, Mungu aliye nguvu yetu;
mpigieni kelele za shangwe Mungu wa Yakobo!
2 Anzeni wimbo, pigeni matari,
pigeni kinubi na zeze kwa sauti nzuri.
3 Pigeni baragumu za pembe za kondoo dume
wakati wa Mwandamo wa Mwezi,
na wakati wa mwezi mpevu,
katika siku ya Sikukuu yetu;
4 hii ni amri kwa Israeli,
agizo la Mungu wa Yakobo.
5 Aliiweka iwe kama sheria kwa Yusufu
alipotoka dhidi ya Misri,
huko tulikosikia lugha ambayo hatukuielewa.
6 Asema, “Nimeondoa mzigo mabegani mwao;
mikono yao iliwekwa huru kutoka kwa kikapu.
7 Katika shida yako uliniita nami nikakuokoa,
nilikujibu katika mawingu yenye ngurumo;
nilikujaribu katika maji ya Meriba.
8 “Enyi watu wangu, sikieni, nami nitawaonya:
laiti kama mngenisikiliza, ee Israeli!
9 Hamtakuwa na mungu mgeni miongoni mwenu;
msimsujudie mungu wa kigeni.
10 Mimi ni Mwenyezi Mungu, Mungu wako,
niliyekutoa nchi ya Misri.
Panua sana kinywa chako
nami nitakijaza.
11 “Lakini watu wangu hawakunisikiliza;
Israeli hakunitii.
12 Basi niliwaacha katika ukaidi wa mioyo yao
wafuate mashauri yao wenyewe.
13 “Laiti watu wangu wangenisikiliza,
laiti Israeli wangefuata njia zangu,
14 ningewatiisha adui zao kwa haraka,
na kuugeuza mkono wangu dhidi ya watesi wao!
15 Wale wanaomchukia Mwenyezi Mungu wangejikunyata mbele zake,
na adhabu yao ingedumu milele.
16 Bali ninyi mngelishwa ngano iliyo bora,
na kuwatosheleza kwa asali inayotoka kwenye mwamba.”