Zaburi 82
Maombi kwa ajili ya kutaka haki 
 Zaburi ya Asafu. 
  1 Mungu anaongoza kusanyiko kuu,  
anatoa hukumu miongoni mwa “miungu”:   
 2 “Hata lini utaendelea kuwatetea wasio haki  
na kuonesha upendeleo kwa waovu?   
 3 Teteeni wanyonge na yatima,  
tunzeni haki za maskini na waliodhulumiwa.   
 4 Mwokoeni mnyonge na mhitaji,  
wakomboeni kutoka mkononi mwa mwovu.   
 5 “Hawajui lolote, hawaelewi lolote.  
Wanatembea gizani;  
misingi yote ya dunia imetikisika.   
 6 “Nilisema, ‘Ninyi ni “miungu”;  
ninyi nyote ni wana wa Aliye Juu Sana.’   
 7 Lakini mtakufa kama wanadamu wa kawaida;  
mtaanguka kama mtawala mwingine yeyote.”   
 8 Ee Mungu, inuka uihukumu nchi,  
kwa kuwa mataifa yote ni urithi wako.