Zaburi 93
Mwenyezi Mungu ni mkuu
Mwenyezi Mungu anatawala, amejivika utukufu;
Mwenyezi Mungu amejivika utukufu
tena amejivika nguvu.
Dunia imewekwa imara,
haitaondoshwa.
Kiti chako cha enzi kimekuwa thabiti tangu zamani;
wewe umekuwa tangu milele.
 
Bahari zimepaza, Ee Mwenyezi Mungu,
bahari zimepaza sauti zake;
bahari zimepaza sauti za mawimbi yake.
Yeye ni mkuu kuliko ngurumo ya maji makuu,
ni mkuu kuliko mawimbi ya bahari:
Mwenyezi Mungu aishiye juu sana ni mkuu.
 
Ee Mwenyezi Mungu, sheria zako ni imara;
utakatifu umepamba nyumba yako
pasipo mwisho.