Zaburi 94
Mwenyezi Mungu, Mlipiza kisasi kwa ajili ya wenye haki
Ee Mwenyezi Mungu, ulipizaye kisasi,
Ee Mungu ulipizaye kisasi, uangaze sasa.
Ee Mhukumu wa dunia, inuka,
uwalipize wenye kiburi kama wanavyostahili.
Ee Mwenyezi Mungu, hadi lini waovu,
hadi lini waovu watashangilia?
 
Wanamimina maneno ya kiburi,
watenda maovu wote wamejaa majivuno.
Ee Mwenyezi Mungu, wanawaponda watu wako;
wanawatesa walio urithi wako.
Wanamchinja mjane na mgeni,
na kuwaua yatima.
Nao husema, “Mwenyezi Mungu haoni,
Mungu wa Yakobo hafahamu.”
 
Sikizeni, enyi wajinga miongoni mwa watu;
enyi wapumbavu, lini mtakuwa na hekima?
Je, aliyeweka sikio asisikie?
Aliyeumba jicho asione?
10 Je, anayeadhibisha mataifa asiadhibu?
Je, awafundishaye wanadamu asiwe na maarifa?
11 Mwenyezi Mungu anajua mawazo ya mwanadamu;
anajua kwamba ni ubatili.
 
12 Ee Mwenyezi Mungu, heri mtu anayeadhibishwa na wewe,
mtu unayemfundisha kwa sheria yako,
13 unampa utulivu siku za shida,
hadi shimo litakapokuwa limechimbwa
kwa ajili ya mwovu.
14 Kwa kuwa Mwenyezi Mungu hatawakataa watu wake,
hatauacha urithi wake.
15 Hukumu itasimamishwa tena kwenye haki,
wote walio na mioyo minyofu wataifuata.
 
16 Ni nani atakayeinuka dhidi ya mwovu kwa ajili yangu?
Ni nani atakayenikinga dhidi ya watenda maovu?
17 Kama Mwenyezi Mungu hangenisaidia upesi,
ningeishi katika kimya cha kifo.
18 Niliposema, “Mguu wangu unateleza,”
Ee Mwenyezi Mungu, upendo wako ulinishikilia.
19 Wasiwasi ulipokuwa mwingi ndani yangu,
faraja yako ilinipa furaha nafsini mwangu.
 
20 Je, kiti cha utawala wa udhalimu kitajiunga nawe,
ule utawala uletao taabu kutokana na sheria zake?
21 Huungana kuwashambulia wenye haki,
kuwahukumu kufa wasio na hatia.
22 Lakini Mwenyezi Mungu amekuwa ngome yangu,
na Mungu wangu amekuwa mwamba ninaoukimbilia.
23 Yeye atawalipa kwa ajili ya dhambi zao
na atawaangamiza kwa ajili ya maovu yao;
Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, atawaangamiza.