Zaburi 96
Mwenyezi Mungu Mfalme mkuu
(1 Nyakati 16:23-33)
1 Mwimbieni Mwenyezi Mungu wimbo mpya;
mwimbieni Mwenyezi Mungu dunia yote.
2 Mwimbieni Mwenyezi Mungu, lisifuni jina lake;
tangazeni wokovu wake siku baada ya siku.
3 Tangazeni utukufu wake katika mataifa,
matendo yake ya ajabu miongoni mwa mataifa yote.
4 Kwa kuwa Mwenyezi Mungu ni mkuu mwenye kustahili kusifiwa kuliko wote;
yeye ni wa kuogopwa kuliko miungu yote.
5 Kwa maana miungu yote ya mataifa ni sanamu,
lakini Mwenyezi Mungu aliziumba mbingu.
6 Fahari na enzi viko mbele yake;
nguvu na utukufu vimo patakatifu pake.
7 Mpeni Mwenyezi Mungu, enyi jamaa za mataifa,
mpeni Mwenyezi Mungu utukufu na nguvu.
8 Mpeni Mwenyezi Mungu utukufu unaostahili jina lake;
leteni sadaka na mje katika nyua zake.
9 Mwabuduni Mwenyezi Mungu katika uzuri wa utakatifu wake;
dunia yote na itetemeke mbele zake.
10 Semeni katika mataifa kwamba, “Mwenyezi Mungu anatawala.”
Ulimwengu ameuweka imara, hauwezi kusogezwa;
atawahukumu watu kwa uadilifu.
11 Mbingu na zishangilie, nchi na ifurahi;
bahari na ivume, na vyote vilivyo ndani yake;
12 mashamba na yashangilie,
pamoja na vyote vilivyomo.
Kisha miti yote ya msituni itaimba kwa furaha;
13 itaimba mbele za Mwenyezi Mungu kwa maana anakuja,
anakuja kuihukumu dunia.
Ataihukumu dunia kwa haki,
na mataifa katika kweli yake.