Zaburi 98
Mwenyezi Mungu Mtawala wa dunia
Zaburi.
Mwimbieni Mwenyezi Mungu wimbo mpya,
kwa maana ametenda mambo ya ajabu;
kitanga chake cha kuume na mkono wake mtakatifu
umemfanyia wokovu.
Mwenyezi Mungu ameufanya wokovu wake ujulikane
na amedhihirisha haki yake kwa mataifa.
Ameukumbuka upendo wake
na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli;
miisho yote ya dunia imeuona
wokovu wa Mungu wetu.
 
Mpigieni Mwenyezi Mungu kelele za shangwe, dunia yote,
ipaze sauti kwa nyimbo za shangwe na vinanda;
mwimbieni Mwenyezi Mungu kwa kinubi,
kwa kinubi na sauti za kuimba,
kwa tarumbeta na mvumo wa baragumu za pembe za kondoo dume:
shangilieni kwa furaha mbele za Mwenyezi Mungu, aliye Mfalme.
 
Bahari na ivume na kila kilicho ndani yake,
dunia na wote wanaoishi ndani yake.
Mito na ipige makofi,
milima na iimbe pamoja kwa furaha,
vyote na viimbe mbele za Mwenyezi Mungu,
kwa maana yuaja kuhukumu dunia.
Atahukumu dunia kwa haki
na mataifa kwa haki.