Zaburi 110
Mwenyezi Mungu na mfalme wake mteule
Zaburi ya Daudi.
1 Mwenyezi Mungu amwambia Bwana wangu:
“Keti mkono wangu wa kuume,
hadi nitakapowafanya adui zako
kuwa mahali pa kuweka miguu yako.”
2 Mwenyezi Mungu ataeneza fimbo yako ya utawala yenye nguvu kutoka Sayuni;
utatawala katikati ya adui zako.
3 Askari wako watajitolea kwa hiari
katika siku yako ya vita.
Ukiwa umevikwa fahari takatifu,
kutoka tumbo la mapambazuko
utapokea umande wa ujana wako*au vijana wako watakujia kama umande.
4 Mwenyezi Mungu ameapa,
naye hatabadilisha mawazo yake:
“Wewe ni kuhani milele,
kwa mfano wa Melkizedeki.”
5 Bwana yuko mkono wako wa kuume,
atawaponda wafalme siku ya ghadhabu yake.
6 Atawahukumu mataifa, akilundika mizoga
na kuwaponda watawala wa dunia nzima.
7 Atakunywa maji katika kijito kando ya njia†au Yeye atoaye mtu wa kurithi mwingine atamweka kwenye mamlaka;;
kwa hiyo atainua kichwa chake juu.
*Zaburi 110:3 au vijana wako watakujia kama umande
†Zaburi 110:7 au Yeye atoaye mtu wa kurithi mwingine atamweka kwenye mamlaka;