Zaburi 115
Mwenyezi Mungu Mmoja wa kweli
1 Sio kwetu sisi, Ee Mwenyezi Mungu, sio kwetu sisi,
bali utukufu ni kwa jina lako,
kwa sababu ya upendo
na uaminifu wako.
2 Kwa nini mataifa waseme,
“Yuko wapi Mungu wao?”
3 Mungu wetu yuko mbinguni,
naye hufanya lolote limpendezalo.
4 Lakini sanamu zao ni za fedha na dhahabu,
zilizotengenezwa kwa mikono ya wanadamu.
5 Zina vinywa, lakini haziwezi kusema,
zina macho, lakini haziwezi kuona;
6 zina masikio, lakini haziwezi kusikia,
zina pua, lakini haziwezi kunusa;
7 zina mikono, lakini haziwezi kupapasa,
zina miguu, lakini haziwezi kutembea;
wala koo zao haziwezi kutoa sauti.
8 Wale wanaozitengeneza watafanana nazo,
vivyo hivyo wale wote wanaozitumainia.
9 Ee nyumba ya Israeli, mtumainini Mwenyezi Mungu,
yeye ni msaada na ngao yao.
10 Ee nyumba ya Haruni, mtumainini Mwenyezi Mungu,
yeye ni msaada na ngao yao.
11 Ninyi mnaomcha, mtumainini Mwenyezi Mungu,
yeye ni msaada na ngao yao.
12 Mwenyezi Mungu anatukumbuka na atatubariki:
ataibariki nyumba ya Israeli,
ataibariki nyumba ya Haruni,
13 atawabariki wale wanaomcha Mwenyezi Mungu,
wadogo kwa wakubwa.
14 Mwenyezi Mungu na awawezeshe kuongezeka,
ninyi na watoto wenu.
15 Mbarikiwe na Mwenyezi Mungu
Muumba wa mbingu na dunia.
16 Mbingu zilizo juu sana ni mali ya Mwenyezi Mungu,
lakini dunia amempa mwanadamu.
17 Sio wafu wanaomsifu Mwenyezi Mungu,
wale wanaoshuka mahali pa kimya*mahali pa kimya maana yake Kuzimu; kwa Kiebrania ni Sheol.,
18 bali ni sisi tunaomtukuza Mwenyezi Mungu,
sasa na hata milele.
Msifuni Mwenyezi Mungu.†kwa Kiebrania ni Hallelu Yah.
*Zaburi 115:17 mahali pa kimya maana yake Kuzimu; kwa Kiebrania ni Sheol.
†Zaburi 115:18 kwa Kiebrania ni Hallelu Yah.