Zaburi 118
Shukrani kwa ajili ya ushindi
Mshukuruni Mwenyezi Mungu, kwa kuwa ni mwema;
fadhili zake zadumu milele.
 
Israeli na aseme sasa:
“Fadhili zake zadumu milele.”
Nyumba ya Haruni na iseme sasa:
“Fadhili zake zadumu milele.”
Wote wanaomcha Mwenyezi Mungu na waseme sasa:
“Fadhili zake zadumu milele.”
 
Wakati wa maumivu yangu makuu, nilimlilia Mwenyezi Mungu,
naye akanijibu kwa kuniweka huru.
Mwenyezi Mungu yuko pamoja nami, sitaogopa.
Mwanadamu anaweza kunitenda nini?
Mwenyezi Mungu yuko pamoja nami,
yeye ni msaidizi wangu.
Nitawatazama adui zangu
wakiwa wameshindwa.
 
Ni bora kumkimbilia Mwenyezi Mungu
kuliko kumtumainia mwanadamu.
Ni bora kumkimbilia Mwenyezi Mungu
kuliko kuwatumainia wakuu.
 
10 Mataifa yote yalinizunguka,
lakini kwa jina la Mwenyezi Mungu naliwakatilia mbali.
11 Walinizunguka pande zote,
lakini kwa jina la Mwenyezi Mungu naliwakatilia mbali.
12 Walinizunguka kama kundi la nyuki,
lakini walikufa haraka kama miiba iteketeayo;
kwa jina la Mwenyezi Mungu naliwakatilia mbali.
 
13 Nilisukumwa nyuma karibu kuanguka,
lakini Mwenyezi Mungu alinisaidia.
14 Mwenyezi Mungu ni nguvu yangu na wimbo wangu,
yeye amefanyika wokovu wangu.
 
15 Sauti za shangwe na ushindi
zinavuma kwenye hema za wenye haki:
“Mkono wa kuume wa Mwenyezi Mungu
umetenda mambo makuu!
16 Mkono wa kuume wa Mwenyezi Mungu
umeinuliwa juu,
mkono wa kuume wa Mwenyezi Mungu
umetenda mambo makuu!”
 
17 Sitakufa, bali nitaishi,
nami nitayatangaza matendo ya Mwenyezi Mungu.
18 Mwenyezi Mungu ameniadhibu vikali,
lakini hakuniacha nife.
 
19 Nifungulie malango ya haki,
nami nitaingia na kumshukuru Mwenyezi Mungu.
20 Hili ni lango la Mwenyezi Mungu
ambalo wenye haki wanaweza kuliingia.
21 Nitakushukuru, kwa kuwa ulinijibu,
umekuwa wokovu wangu.
 
22 Jiwe walilolikataa waashi,
limekuwa jiwe kuu la pembeni.
23 Mwenyezi Mungu ametenda hili,
nalo ni la kushangaza machoni petu.
24 Hii ndiyo siku Mwenyezi Mungu aliyoifanya,
tushangilie na kufurahi ndani yake.
 
25 Ee Mwenyezi Mungu, tuokoe,
Ee Mwenyezi Mungu, utujalie mafanikio.
26 Heri yule ajaye kwa jina la Mwenyezi Mungu.
Kutoka nyumba ya Mwenyezi Mungu tunakubariki.
27 Mwenyezi Mungu ndiye Mungu,
naye ametuangazia nuru yake.
Mkiwa na matawi mkononi,
unganeni kwenye maandamano ya sikukuu
hadi kwenye pembe za madhabahu.
 
28 Wewe ni Mungu wangu, nitakushukuru,
wewe ni Mungu wangu, nitakutukuza.
 
29 Mshukuruni Mwenyezi Mungu kwa kuwa ni mwema;
fadhili zake zadumu milele.