Zaburi 120
Kuomba msaada dhidi ya wadanganyifu
Wimbo wa kwenda juu.
1 Katika dhiki yangu namwita Mwenyezi Mungu,
naye hunijibu.
2 Ee Mwenyezi Mungu, uniokoe kutoka midomo ya uongo
na ndimi za udanganyifu.
3 Atakufanyia nini,
au akufanyie nini zaidi, ewe ulimi mdanganyifu?
4 Atakuadhibu kwa mishale mikali ya shujaa,
kwa makaa yanayowaka ya mti wa mretemu.
5 Ole wangu kwa kuwa naishi Mesheki,
kwamba naishi katikati ya mahema ya Kedari!
6 Nimeishi muda mrefu mno
miongoni mwa wale wanaochukia amani.
7 Mimi ni mtu wa amani;
lakini ninaposema, wao wanataka vita.