Zaburi 121
Mwenyezi Mungu mlinzi wetu
Wimbo wa kwenda juu.
Nayainua macho yangu natazama milima:
msaada wangu utatoka wapi?
Msaada wangu hutoka kwa Mwenyezi Mungu,
Muumba wa mbingu na dunia.
 
Hatauacha mguu wako uteleze,
yeye akulindaye hatasinzia,
hakika, yeye alindaye Israeli
hatasinzia wala hatalala usingizi.
Mwenyezi Mungu anakulinda,
Mwenyezi Mungu ni uvuli wako mkono wako wa kuume,
jua halitakudhuru mchana,
wala mwezi wakati wa usiku.
Mwenyezi Mungu atakukinga na madhara yote,
atayalinda maisha yako,
Mwenyezi Mungu atakulinda unapoingia na unapotoka,
tangu sasa na hata milele.