Zaburi 122
Sifa kwa Yerusalemu
Wimbo wa kwenda juu. Wa Daudi.
Nilishangilia pamoja na wale walioniambia,
“Twende nyumbani mwa Mwenyezi Mungu.”
Ee Yerusalemu, miguu yetu imesimama
malangoni mwako.
 
Yerusalemu imejengwa vyema kama mji
ulioshikamana pamoja.
Huko ndiko makabila hukwea,
makabila ya Mwenyezi Mungu,
kulisifu jina la Mwenyezi Mungu kulingana na maagizo
waliopewa Israeli.
Huko viti vya hukumu hukaa,
viti vya ufalme vya nyumba ya Daudi.
 
Omba kwa ajili ya amani ya Yerusalemu:
“Wote wanaokupenda na wawe salama.
Amani na iwe ndani ya kuta zako,
na usalama ndani ya ngome zako.”
Kwa ajili ya ndugu na rafiki zangu,
nitasema, “Amani iwe ndani yako.”
Kwa ajili ya nyumba ya Mwenyezi Mungu, Mungu wetu,
nitatafuta mafanikio yako.