Zaburi 123
Kuomba rehema
Wimbo wa kwenda juu.
1 Ninayainua macho yangu kwako,
kwako wewe unayeketi mbinguni kwenye kiti chako cha enzi.
2 Kama vile macho ya watumwa
yatazamavyo mkono wa bwana wao,
kama vile macho ya mjakazi
yatazamavyo mkono wa bibi yake,
ndivyo macho yetu yamtazamavyo Mwenyezi Mungu, Mungu wetu,
hadi atakapotuhurumia.
3 Uturehemu, Ee Mwenyezi Mungu, uturehemu,
kwa maana tumevumilia dharau nyingi.
4 Tumevumilia dhihaka nyingi kutoka kwa wenye kiburi,
dharau nyingi kutoka kwa wenye majivuno.