Zaburi 124
Shukrani kwa ukombozi wa Israeli
Wimbo wa kwenda juu. Wa Daudi.
Kama Mwenyezi Mungu hangekuwa upande wetu;
Israeli na aseme sasa:
kama Mwenyezi Mungu hangekuwa upande wetu,
watu walipotushambulia,
hasira yao ilipowaka dhidi yetu,
wangetumeza tukiwa hai,
mafuriko yangegharikisha,
maji mengi yangetufunika,
maji yaendayo kasi
yangetuchukua.
 
Ahimidiwe Mwenyezi Mungu,
ambaye hakuruhusu turaruliwe kwa meno yao.
Tumeponyoka kama ndege
kutoka mtego wa mwindaji;
mtego umevunjika,
nasi tumeokoka.
Msaada wetu ni katika jina la Mwenyezi Mungu,
Muumba wa mbingu na dunia.